Alhamisi, 11 Agosti 2016

Serikali yalifungia Gazeti la Mseto kwa Kuchapisha Habari za Uongo

Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu kulifungia gazeti la Mseto kwa miezi 36 leo Agosti 11,2016 katika ukumbi wa Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
“Serikali kwa masikitiko makubwa imelazimika kilifungia gazeti la Mseto  kutokana na mwenendo wa uandishi wa kuandika na kuchapisha habari za uongo na kugushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais  wetu wa Awamu ya Tano  Mhe.Dkt.John Pombe Mgufuli na viongozi wa Serikali” Alisema Mhe Waziri Nape.

Aidha Mhe. Nape amesema kuwa hatua ya kulifungia gazeti la Mseto imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda  mrefu kuanzia Septemba,2012 hadi Agosti,2016 kumtaka Mhariri wa gazeti hilo kuacha kuandika  habari za upotoshaji,uchochezi na za uongo na zisizo zingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa Habari bila mafanikio.

Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayoanisha Uhuru wa Habari na mipaka ya habari kama vile tamko la Haki za Binaadamu la mwaka 1948 ambapo nchi yetu imeruhusu kwa kiwango kikubwa  kwa kuweka ukomo wa uhuru huo kwa kukataza habari za uzushi uongo na uchochezi.
Gazeti la Mseto limezuiwa kuchapishwa katika njia nyingine yeyote ikiwemo mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya  Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu kulifungia gazeti la Mseto kwa miezi 36 leo Agosti 11,2016 katika ukumbi wa Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari MAELEZO Bw.Vicent Tiganya.   

0 maoni:

Chapisha Maoni