Mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi
Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu ameliasa jeshi la polisi
Wilayani humo kutofanya kazi kwa mazoea badala yake kuimarisha ulinzi na
usalama wa raia na mali zao.
Mtaturu
ameyasema hayo wakati wa kikao cha pamoja na askari wa jeshi hilo
Wilayani humo ikiwa ni ziara yake ya mwanzo kudhuru katika ofisi za
makao makuu ya Jeshi hilo kwa ajili ya kujionea hali ya utendaji wa
askari hao sawia na kukagua ofisi hizo ili kujua changamoto
zinazowakabili katika utendaji wao.
Mkuu
huyo wa Wilaya amesema kuwa kitendo cha baadhi ya askari kupokea Rushwa
kutoka kwa wananchi ni miongoni mwa sababu zinazopelekea wananchi
kukosa imani na serikali na kulipaka matope jeshi hilo ikiwa ni pamoja
na kuifanya serikali ionekane haifanyi kazi yake ipasavyo.
“Hakuna
asiyetambua kuwa Rushwa ni adui wa haki hivyo nawasihi askari
wapambanaji kutochukua Rushwa ili kuifanya jamii kuwa na imani na askari
wao jambo hilo litaongeza heshima kwenu na kwa serikali kwa ujumla,
lakini mnapaswa kutambua kuwa kupokea Rushwa kunasababisha wananchi
kujichukulia sheria mkononi jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa nchi
yetu,” alisema Mtaturu
Mtaturu
alisema kuwa Jeshi la Polisi ni sehemu ya ukombozi wa Taifa pia ni
sehemu muhimu ya kuimarisha usalama wa Wananchi, hivyo ikifikia hatua
wananchi wanakosa imani na jeshi la polisi ni wazi kuwa nchi itakuwa
inaelekea mahali ambapo sio sahihi.
Pamoja
na mambo mengine Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa serikali inatambua
kuwa kuna upungufu wa nyumba za kuishi askari, vifaa vya utendaji kazi,
Pamoja na mazingira na miundombinu kuwa duni hivyo serikali imejipanga
kuimarisha kadhia hizo kwa Jeshi la Polisi ambapo tayari kuelekea kwenye
maboresho wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es salaam kuwa eneo la mfano
(Pilot Area) ili kuondoa changamoto hizo.
Dc
Mtaturu ametoa mwito kwa askari hao kuwashirikisha wananchi kwa kiasi
kikubwa pale inapobidi ili kupunguza sintofahamu iliyopo katika jamii ya
askari kufanya kazi wenyewe pasina kushirikisha Raia kikamilifu.
“Nina
amini katika utendaji wa ushirikishwaji kwa wananchi kufanya hivyo ni
kuwasaidia wananchi kupunguza hisia hasi walizonazo juu ya utendaji wa
Jeshi la Polisi, lakini pia nawaomba mfanye upelelezi kwa haraka kwa
kesi zilizopo mezani kwenu ili kurahisisha kupunguza mlundikano wa kesi
jambo linalopelekea kutotendewa haki kwa baadhi ya wananchi,” alisema
Mtaturu
Kikao
cha pamoja kati ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na Askari wa Jeshi la
Polisi Wilayani humo kilikuwa na taswira chanya ya kufahamiana,
kuimarisha umoja kiutendaji pamoja na kukumbushana majukumu ya kazi.
Mkuu
huyo wa Wilaya ya ikungi pia amewapongeza askari hao pamoja na
mazingira magumu waliyonayo lakini wanafanya kazi vizuri kwa mujibu wa
viapo vyao.
Na Mathias Canal, Singida
0 maoni:
Chapisha Maoni