Na Veronica Simba
Serikali
ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini hususan
katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya miwa. Hayo
yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Brazil nchini
Tanzania, Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo
naye.
Balozi
Puente alimweleza Profesa Muhongo kuwa nchi yake inao ujuzi na uzoefu
wa kutosha katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali
hususan maji.
Alisema, Brazil ingependa kuchangia kufanikisha azma ya Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda, unahitaji umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba Tanzania inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.
Alisema
kuwa, nchini Brazil, kuna Kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda mrefu
unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi hiyo, ambazo huzalisha umeme wa
maji nchini mwao na hata nje ya nchi.
Pia,
alitaja eneo jingine ambalo nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni
uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya miwa ambayo aliielezea kuwa
chanzo kizuri cha nishati safi.
Balozi
Puente alisisitiza kuwa, Brazil ikiwa ni nchi inayozalisha miwa kwa
kiwango kikubwa duniani, itasaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya
nishati kwa kuzalisha umeme unaotokana na mabaki ya miwa kwa kutumia
teknolojia za kisasa.
Kwa
upande wake, Waziri Muhongo, akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa kuwa
Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo mkubwa hususan katika maeneo ambayo
Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi hiyo inakaribishwa kuwekeza
Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu uliowekwa na Serikali.
Akizungumzia
zaidi kuhusu utaratibu wa uwekezaji, Waziri Muhongo alieleza kwamba
Serikali ya Tanzania, kupitia Wizara yake, inabadilisha utaratibu wa
kupokea wawekezaji katika sekta husika.
Alisema,
kunaandaliwa utaratibu maalum utakaokuwa wa wazi na kuruhusu ushindani
kwa wenye nia ya kuwekeza kwa malengo ya kupunguza au kuondoa kabisa
mazingira ya rushwa na muda mrefu unaotumika katika majadiliano pasipo
sababu za msingi.
Profesa
Muhongo alifafanua zaidi kwamba, Serikali itaweka mazingira mazuri
zaidi ya ushindani kwa kuandaa maelezo ambayo pamoja na mambo mengine
yatabainisha aina mbalimbali za vyanzo vya umeme vilivyopo nchini pamoja
na maeneo vilipo.
Alisema,
Kampuni zenye nia ya kuwekeza zitakaribishwa kupendekeza viwango vya
bei vitakavyotumika kuuza umeme utakaozalishwa na zitashindanishwa,
ambapo washindi wachache watachaguliwa kwa ajili ya majadiliano kabla ya
kuingia mkataba wa uwekezaji husika.
“Kwa hivyo, tunaandaa kabrasha maalum litakalokuwa na maelezo husika na litakuwa tayari mwezi wa Septemba mwaka huu. Kabrasha hilo lenye maelezo litatumika kama mwongozo wa ushindanishaji maombi mbalimbali ya uwekezaji hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kwa uwazi,” alisisitiza.
Alivitaja
vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na gesi asilia, makaa ya mawe, maji, jua,
upepo, jotoardhi, mawimbi ya bahari pamoja na nishati mbadala. Waziri
Muhongo alisema kuwa maelezo hayo maalum yatasambazwa kwa wadau
mbalimbali wa sekta husika wakiwemo wale wote wenye nia ya kuwekeza
ikiwa ni pamoja nan chi ya Brazil kupitia Ubalozi wake hapa nchini.
“Kwa kutumia Kabrasha hilo maalum lenye maelezo husika, wewe Balozi utaweza kuwashawishi wafanyabiashara kutoka nchini kwako kutoa mapendekezo ya uwekezaji ambayo yana vigezo vyote muhimu vinavyoshawishi wapate fursa husika za uwekezaji katika sekta ya nishati,” Profesa Muhongo alimweleza Balozi Puente.
Kuhusu
Mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda
hadi Tanzania, ambao pia Brazil imeonesha nia kuwa ingependa kuwekeza
kwa kushirikiana na Tanzania; Profesa Muhongo alisema Serikali itaweza
kulisemea hilo baada ya kipindi cha miezi takribani 45 kupita, ambapo
mambo yote ya kisheria kuhusu Mradi huo yanatarajiwa kuwa yamekamilika.
Aidha,
Profesa Muhongo alitumia fursa hiyo kuomba nafasi za masomo nchini
Brazil kwa wanafunzi wa kitanzania katika ngazi za Shahada za Uzamili na
Uzamivu katika sekta ya Nishati hususan Mafuta na Gesi, kwa kuzingatia
kuwa Brazil imeendelea sana katika sekta hiyo.
“Ninyi mnazo Taasisi bora kabisa za Utafiti duniani. Mnafanya vizuri sana katika maeneo mbalimbali.”
Kwa
mujibu wa Profesa Muhongo, Brazil ni miongoni mwa nchi Tano (5) bora
duniani zinazozalisha umeme kwa kutumia nishati jadidifu kwa sababu
umeme mwingi wanaozalisha unatokana na maji, kutoka katika Mito mikubwa
waliyonayo.
Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (Kushoto), akisaini Kitabu cha Wageni ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia), alipomtembelea Waziri na kufanya naye mazungumzo kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hususan katika uwekezaji kwenye sekta ya nishati.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto), akimsikiliza kwa makini Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente (kulia), wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri Ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni na kufanya mazungumzo naye kuhusu masuala ya uwekezaji katika sekta za nishati na madini. Wengine pichani ni Maafisa wa Wizara waliohudhuria mkutano huo.
0 maoni:
Chapisha Maoni