Alhamisi, 11 Agosti 2016

WATOTO WENYE UMRI CHINI YA MIAKA MITANO HATARINI KUFA KWA KUKOSA DAMU

Kamanda wa jeshi la zima moto na uokoaji mkoani Pwani, mrakibu msaidizi,Goodluck Zerote ,akichangia damu ,katika zoezi lililoendeshwa na jeshi hilo ,kuchangia damu hospital ya rufaa ya Tumbi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WATOTO chini ya umri wa miaka mitano mkoani Pwani wako kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa damu.

Hayo yalielezwa na afisa muuguzi wa wa kitengo cha damu salama hosptali ya rufaa ya Tumbi ,Elisia Towo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya zoezi la utoaji damu kwa hiari lililokuwa likiendeshwa na jeshi la zima moto na uokoaji mkoani hapo.

Alisema watoto wenye umri huo wamekuwa wakiongoza kwa kukosa damu kutokana kuugua ugonjwa wa malaria lakini pia kucheleweshwa kuwahishwa hospitali mapema.

"Tumekuwa tukiwahamasisha wazazi katika mihadhara mbalimbali kuhakikisha wanawawahisha watoto hosptali pindi wanapoona dalili ya  homa ama malaria badala ya kuwaleta wakiwa wameshachoka na ugonjwa”, alisema Towo.

Alieleza kuwa kundi jingine lililo hatarini ni wakina mama wajawazito ambao nao wamekuwa wakipata tatizo la ukosefu wa damu ama wakihitaji kufanyiwa upasuaji .
Towo amesema watu wengine ni majeruhi wa ajali ambao hawatabiriki kwani ajali hutokea bila ya kuwa na taarifa.

Muuguzi huyo alisema kutokana na mahitaji hayo hosptali ya rufaa ya Tumbi inahitaji damu nyingi zaidi ambapo kwa sasa iliyopo  ni unit 25 ambayo ni ndogo ikilinganishwa na matukio ya mara kwa mara ya ajali.

“Kwa siku tunakusanya unit 12 hadi 20 na mahitaji yetu kwa mwezi ni kuanzia unit 250 hadi 300, bado damu haitoshi, nawaomba wananchi wa mkoa wa Pwani wajitokeze kuchangia damu kwa hiari ili waweze kuokoa maisha ya watanzania wenzetu wanaohitaji damu”, alisema Towo.

Afisa uhusiano wa  jeshi la zima moto na uokoaji SGT Harrison Mkonyi alisema zoezi hilo ni endelevu na kuwa lengo ni kuhakikisha jeshi hilo linatimiza kauli mbiu yake ya kuokoa maisha na mali kwa vitendo.

Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Pwani  Mrakibu msaidizi Gudluck Zerote ,alisema hii ni mara ya kwanza kwa jeshi hilo mkoani humo kuchangia damu.

Kamanda Zerote alisema kutokana na kuwa kwa mara ya kwanza  wamechangia damu hosptali ya Tumbi unit 12, na kuwa watachangia  baada ya miezi mitatu.

0 maoni:

Chapisha Maoni