Hussein Makame-MAELEZO
Jumla ya washitakiwa 572
wamepatikana na hatia kufuatia tuhuma za rushwa zilizowakabili katika
mahakama mbalimbali nchini katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishna
Valentino Mlowola katika taarifa iliyotolewa kwa niaba yake na Afisa
habari wa taasisi hiyo Mussa Misalaba.
Taarifa hiyo inaonesha kuongezeka
kwa idadi ya washitakiwa waliopatikana na hatia ambapo mwaka 2010
washitakiwa 61 walitiwa hatiani wakati hadi kufikia Desemba 2015
mahakama iliwatia hatiani washitakiwa 188.
Alisema katika mwaka 2015
(Januari-Desemba) jumla ya matukio ya rushwa 5,000 yaliripotiwa na aina
ya rushwa iliyoripotiwa mara nyingi ni matumizi mabaya ya madaraka.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa katika
kipindi hicho cha miaka 6 kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, kesi mpya 1,691
zilizofikishwa mahakamani zikiwemo kesi 227 zilizofikishwa mwaka 2010,
kesi 193 (2011), kesi 288 (2012), kesi 343 (2013), kesi 256 (2014) huku
kesi 384 zikifikishwa mahakamani mwaka 2015.
Aliongeza kuwa kesi zilizokuwa
zinaendelea mahakamani kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 zilikuwa 3,321 huku
washitakiwa walioachiwa huru na mahakama katika kipindi hicho wakiwa
646.
Kwa upande wa kesi za rushwa
zilizoondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali kuanzia mwaka
2010 hadi 2015 zilikuwa 162 kati ya hizo mwaka 2010 zilikuwa kesi 30,
mwaka 2011 kesi 26 na mwaka 2012 kesi 24.
Kwa mwaka 2013 kulikuwa na kesi 17 zilizoondolewa mahakamani,wakati mwaka 2014 zilikuwa kesi 33 huku mwaka 2015 zikiwa kesi 32.
Mbali na kesi hizo, Kamishna Mlowola alisema kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 kesi 54 zilikatiwa.
Kamishna Mlowola alimtaka kila
mwananchi kutekeleza jukumu lake la kikatiba na kisheria katika kuzuia
na kupambana na vitendo vya rushwa nchini.
Kifungu cha 39 cha Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kinatamka kuwa
“kila mtu anayefahamu kutendeka kwa kosa au anafahamu kusudio la mtu
mwingine kutenda kosa chini ya Sheria hii anatakiwa kutoa taarifa
TAKUKURU”.
“Hivyo, tunamsihi kila Mtanzania
asijiingize katika vitendo vya rushwa na asinyamaze anapofahamu
kutendeka kwa vitendo hivyo au hata kuwa na wasiwasi na mali
zinazomilikiwa na mtu yeyote.” Alisema.
Alifafanua kuwa njia mojawapo
nyepesi ya kuifikia TAKUKURU ni kupiga simu bure kwenda namba 113 au
*113# (USSD) na kutoa taarifa za rushwa kwa muda wote wa saa 24.
Akizungumzia jinsi ya kukabiliana
na vitendo vya rushwa, Kamishna Mlowola alisema ni wajibu kwa kila
mwananchi kuzuia rushwa kwa kujijengea uelewa wa taratibu za eneo
analokwenda kupata huduma na kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa za
vitendo vya rushwa vinavyotokea au vilivyotokea ili hatua za kisheria
zichukuliwe.
0 maoni:
Chapisha Maoni