MKUU wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida,Geofrey Idelfonce Mwambe,amewaagiza walimu wa shule za msingi na sekondari wahakikishe samani ikiwemo madawati yanatunza vizuri,vinginevyo watakatwa sehemu ya mishahara yao, endapo yataharibika au kuvunjwa.
Mkuu huyo wa wilaya,ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi madawati 100 kwa shule za msingi za Bangayegya na Lulanga za halmashauri ya wilaya ya Itigi.Madawati hayo yametolewa msaada na benki ya NMB tawi la Itigi.
Alisema madawati na samani zingine zote,zinapaswa kulindwa na kutunzwa vizuri,ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
“Kumkata mshahara mwalimu ambaye anafanya kazi katika mazingira magumu,haipendezi hata kidogo.Lakini tunalazimika kufanya hivyo, kama njia mojawapo ya kudhibiti uharibifu wa madawati.Kwa hali hiyo,wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ya Itigi na Manyoni, simamieni hili agizo hili”, alisema mkuu huyo wa wilaya.
Meneja NMB kanda ya kati,Straton Chilongola
Meneja NMB kanda ya kati, Straton Chilongola,akitoa taarifa yake kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 50 kwa shule ya msingi Bangayegya Itigi. NMB tawi la Itigi limetoa msaada wa madawati 100 kwa shule za msingi ya Bangayegya na Lulanga yenye thamani ya shilini milioni 10. Anayeangalia kamera ni Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Geofrey Mwambe, Meneja wa NMB tawi la Itigi,Victor Dilunga (wa kwanza kulia) na Mwenyekiti wa halmashauri ya Itigi, Alli Minja (wa tatu kulia).(Picha na Nathaniel Limu, Manyoni)
Aidha,Mwambe ameagiza wanafunzi kusoma kwa bidii kubwa, ili waweze kufanya vizuri kwenye mitihani yao na akadai kwamba kitendo hicho kitawavutia zaidi wafadhili na wadau wengine wa sekta ya elimu, kuendelea kutoa misaada mbalimbali.
“Walimu wa shule za msingi na sekondari….ongezeni bidii katika kutekeleza majukumu yenu ya kufundisha.Kipaumbele changu ni kwamba nataka au natarajia ufaulu ufikie asilimia 98.Elimu bora ndiyo itakayosaidia kwa mfano, baadhi ya watoto wa shule ya msingi Lulanga wasome na baadaye wawe wakuu wa wilaya,mikoa au marubani wa ndege.Hilo linawezekana kabisa.”,alifafanua.
Mwambe alitumia fursa hiyo kuishukuru na kuipongeza benki ya NMB tawi la Itigi, kwa msaada huo wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10.
“Kwa kitendo hiki,NMB mmeiunga mkono serikali ya awamu ya tano katika mapambano yake ya kumaliza tatizo la uhaba wa madawati nchini.Naomba na taasisi zingine na wadau mbalimbali,wainge mfano huu wa NMB katika kuiunga mkono serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu”,alisema mkuu huyo wa wilaya.
Mkuu wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe
Mkuu wa wilaya ya Manyoni, Geofrey Mwambe, akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 50 kwa shule ya msingi ya Lulanga halmashauri ya wilaya ya Itigi yaliyotolewa msaada na NMB Itigi. Pamoja na mambo mengine, Mwambe alionya kwamba dawati likiharibika, mwalimu husika atapaswa kukatwa mshahara wake,ili kugharamia uharibifu wa dawati/madawati. Wengine katika picha Meneja NMB kanda ya kati,Straton Chilongola (wa tatu kulia), Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Itigi,Alli Minja (wa kwanza kulia)  na anayefuata ni Meneja NMB tawi la Itigi,Victor Dilunga pamoja na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Itigi, Pius Shinja Luhende (wa kwanza kushoto).
Katika hatua nyingine,Mwambe alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi na hasa vijana, kujenga utamaduni wa kuweka akiba zao za fedha kwenye taasisi za fedha, ikiwemo benki ya NMB.Amedai kwa njia hiyo,fedha zao zitakuwa salama tofauti na zikihifadhiwa majumbani.
Kwa upande wake Meneja wa NMB kanda ya kati,Straton Chilongola,alisema NMB katika mipango yake,imekuwa ikishiriki shughuli mbalimbali za kijamii,husasani kwenye sekta ya elimu,afya na pia kufariji jamii pindi wanapopatwa na majanga kama mafuriko na ajali za barabarani.
“Kwa mwaka huu,NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi kwenye sekta ya elimu na afya.Kiasi hiki kinatufanya kuwa benki  ya kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yo yote nchini”,alisema kwa kujiamini.
Aidha,Chilongola ametumia fursa hiyo, kuwahimiza walimu wakuu wa shule za msingi Bangayegya,  Lulanga na wenyeviti wa kamati za shule,kuhakikisha shule hizo zinapata mafanikio ya hali ya juu kielimu na hivyo, kuwa mfano bora hapa nchini.
Naye Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lulanga,Omari Pumzi, ameishukuru benki ya NMB kwa msaada wake wa madawati 50 kwa shule yake,na kudai kitendo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida
Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida ,Geofrey Mwambe akikata utepe kuashiria makabidhiano ya madawati 50 msaada kutoka NMB tawi la Itigi kwa shule ya msingi Bangayegya,yenye thamani ya shilingi milioni tano.
Straton Chilongola
Meneja NMB kanda ya kati, Straton Chilongola (kushoto) akimkabidhi kuu wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe msaada wa  madawati 50 msaada kutoka NMB tawi la Itigi kwa shule ya msingi Bangayegya,yenye thamani ya shilingi milioni tano.
IMG_7615
Meneja NMB kanda ya kati, Straton Chilongola (kushoto) akimkabidhi kuu wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe msaada wa  madawati 100  msaada kutoka NMB tawi la Itigi kwa shule ya msingi Bangayegya na Lulanga yenye thamani ya shilingi milioni kumi.Hafla hiyo imefanyika kwa nyakati tofauti kwenye shule hizo.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Lulanga
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Lulanga kata ya Itagata halmashauri ya wilaya ya Itigi mkoani Singida, wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Mnayoni mkoani Singida, Geofrey Mwambe wakati akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya msaada wa madawati 50 kutoka NMB tawi la Itigi.(Picha na Nathaniel Limu).