Ukiritimba katika soka ngazi za mikoa limekua ni tatizo kubwa sana  ambalo linapelekea kupotea vipaji vingi katika soka la Bongo (Tanzania)  hasa katika kikanda katika  ngazi za uongozi  yaani Kanda ya kati, Kanda ya Ziwa na Kanda zingine.
Uchunguzi maalum uliofanywa na Mwandishi wa mtandao huu wa Modewjiblog, amebainisha kuwa, katika ngazi hizo za Kanda, vipo vipaji vingi sana katika soka  lakini uongozi mbaya na ukiritimba huvifanya vipaji hivi kupotea katika mazingira ambayo kama viongozi wangetenda wajibu wao basi vipaji hivi vingewez kufika mbali zaidi ya hatua kama Ligi kuu na ligi za nje.
DOREFA-Dodoma:
Kwa  kuangalia kwa undani Mkoa wa Dodoma kupitia chama cha Soka cha Mkoa huo (DOREFA) ni moja katika ngazi za kiuongozi  wa soka katika mkoa wa Dodoma. Mkoa  ambao unaongoza kuzalisha wachezaji wengi na wenye vipaji mahiri vya soka  kama akina Boniphace Pawasa, Idrissa Rashid, Othman iddi Chuji, John Kanakamfumu na wengine wengi  wakiwemo wanaoshiriki  ligi kuu na ligi zingine za ndani na nje ya nchi.
Mbali na hao wapo wachezaji wa soka wengi ambao kimsingi wanafanyiwa ndivyo sivyo ambayo inapelekea vipaji vyao katika kulisakata kabumbu kupotea. Hii hutokana na kukosa malezi bora ya kisoka kwa wachezaji hawa wachanga, pia ni ukiritimba unaofanywa na viongozi ambao wanatamaa za pesa na uongozi.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, yapo matukio mbalimbali katika soka la Mkoa wa Dodoma ambapo wachezaji hawa wachanga wanajikuta katika mazingira magumu ya kuonyesha vipaji vyao pale ambapo viongozi washirikisho la soka wanawabanIa na kuwakatiza nia na tama zao na mchezo wa soka.
Zipo nyakati kama za ligi ya Copa cocacola, ligi ya Vodacom ngazi ya mkoa, ligi za timu daraja la kwanza ambapo wachezaji wengi wenye vipaji hawafiki kokote na vipaji vyao. Hii hutokana na kubaniwa ama kunyimwa kutoka nje ya mkoa huo na timu husika ili kuweza kuonyesha vipaji vyao vya kucheza soka.
Yapo matukio kama wachezaji wa umri chini ya miaka 18 wanaocheza Copa  Coca cola kubaniwa kucheza mashindano ya kikanda ambayo huwa yanafanyika mkoani Dar es salaam, kwa vigezo ambavyo havipo kwenye kanuni za utuzi za kisoka na kiuongozi kwa ujumla.
Miongoni mwa mambo yaliyobainika ni pamoja na Viongozi wa ngazi ya kimkoa huwachagua vijana waliofuzu kushiriki mashindano kindugu na kwa kujuana na wazazi wao, ama huwachagua watoto wao kushiriki michuano mbalimbali bila kuzingatia mfumo sahihi wa uteuzi wa wachezaji na kuzingatia kanuni na taratibu za uongozi.
Itaendelea chapisho lijalo sehemu ya pili.
Na Hashim Ibrahim  (Modewjiblog)
LIGI