Alhamisi, 4 Agosti 2016

UGONJWA WA KISUKARI NA ATHARI ZAKE

Ugonjwa wa kisukari au Kisukari kama kilivyozoeleka miongoni mwetu, ni ugonjwa utokanao na kiwango kikubwa cha sukari katika damu. Sukari katika damu hutokana na kumeng’enywa kwa wanga (carbohydrate).

Kwa kawaida sukari katika damu hukupa nishati ambayo hukuwezesha kutembea, kukimbia, kuendesha baiskeli, kufanya mazoezi na kufanya shughuli zako za kila siku.Insulini ni homoni ibadilishayo sukari iliyoko kwenye damu kuwa nishati.Homoni hii hutengenezwa na aina ya seli ziitwazo beta (beta cells) ambazo hupatikana kwenye kongosho (pancreas).Insulini ni moja kati ya homoni zihusikazo na usimamizi wa kiwango cha sukari katika damu.Kwa mfano, endapo kiwango cha sukari katika damu kitapanda, insulini hufanya kazi ya kukipunguza kufikia kiwango cha kawaida kitakiwacho kwenye mwili wa binadamu mwenye afya njema.Hufanya hivyo kwa kuruhusu sukari iliyopo kwenye damu kuingia kwenye ini, misuli na seli za mafuta (fat cells) ambako hutumika kama nishati.

Mtu mwenye kisukari ni yule ambaye ama mwili wake umeshindwa kutengeneza insulini au kiwango cha insulini ni kidogo kuliko mahitaji yake au mwili umeshindwa kutumia insulini iliyopo.

Kwa nini watu hupata kisukari?

Awali ya yote ni vema ukafahamu kwamba kuna aina mbili kuu za kisukari.Aina ya kwanza ni ile ya kisukari kitegemeacho insulini (Insulin Dependent Diabetes Mellitus) na nyingine ni kisukari kisichotegemea insulini (Non Insulin Dependent Diabetes Mellitus). Baadhi ya vyanzo hujumuisha Kisukari kitokanacho na Ujauzito (Gestational Diabetes) kama aina ya tatu ya kisukari.

(i) Kisukari Kitegemeacho Insulini

Katika aina hii ya kisukari mwili wa binadamu hushindwa ama kutengeneza homoni ya insulini au hutengeneza insulini kidogo sana ambayo hushindwa kusimamia kiwango cha sukari kwenye damu. Kutokana na takwimu za nchini Marekani, aina hii ya kisukari inasemekana kuathiri karibu asilimia kumi (10%) ya wagonjwa wote wa kisukari. Aina hii ambayo kwa kawaida hugundulika utotoni au ujanani, pia yaweza kumtokea mtu mzima endapo kongosho yake imeharibika kutokana na pombe, ugonjwa au kuondolewa kutokana na upasuaji.Watu wenye aina hii ya kisukari kwa ujumla huhitaji matibabu ya kila siku ya insulini ili waendelee kuishi.

Sababu za mtu kupata aina hii ya kisukari ni kama zifuatazo:

Mosi ni sababu za kijenetiki.Hizi huchangia karibu theluthi moja ya uwezekano wa kupata kisukari kitegemeacho insulini.Tafiti mbalimbali zinazohusiana na seli za binadamu zimeonyesha uhusiano mkubwa kati ya aina hii ya kisukari na antijeni za chembe hai nyeupe za binadamu (Human Leucocyte Antigen-HLA) haswa zile za aina ya HLA-DR3 na HLA-DR4 kwa karibu ya asilimia 95 ya wagonjwa.

Sababu ya pili inayohusishwa na aina hii ya kisukari ni iwapo mgonjwa wa kisukari alishawahi kuugua ugonjwa utokanao na virusi.Uthibitisho unapatikana kutokana na tafiti zilizofanywa na ambapo chembechembe za virusi zimegundulika kusababisha madhara dhidi ya kinga ya mwili (autoimmune damage) kwa seli zihusianazo na kinga kudhuru seli zake zenyewe hasa zile za beta zilizopatikana toka kwenye kongosho. Baadhi ya virusi vihusishwavyo ni Rubella, Epstein Barr, Cytomegalovirus, Coxsackie B4 na Mumps; ingawa jinsi virusi hivyo vinavyodhuru bado haijafahamika.

Aina ya mlo ni sababu ya tatu iletayo kisukari kinachotegemea insulini. Aina ya protini ipatikanayo kwenye damu ya ng’ombe na ambayo ni sehemu kubwa inayotengeneza maziwa ya ng’ombe imeonekana kuchokoza uwezekano wa kupata aina hii ya kisukari. Imegundulika kwamba watoto walionyweshwa maziwa ya ng’ombe mapema utotoni wana asilimia kubwa ya kupata aina hii ya kisukari kuliko wale walionyonyeshawa titi la mama.

Msongo wa mawazo pia waweza changia kupata kisukari kinachotegema insulini kwa kuchochea mwili kutengeneza homoni zipinganazo na hali ya msongo wa mawazo.

Aina hii ya kisukari huwa na sifa zifuatazo:
Huanza kabla ya mtu kufikisha umri wa miaka arobaini, umbile la mwili huwa la kawaida au hupungua (kukonda), kiwango cha insulini kwenye damu huwa chini wakati kiwango cha glukagoni (homoni ibadilishayo glaikojeni kuwa sukari) huwa juu.

Dalili zake huonekana mapema kama kuwa na kiu sana, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito mbali ya kula sana, kuchoka choka, kichafuchefu na kutapika.

(ii) Kisukari kinachotegemea insulini

Aina hii ya pili ya kisukari hutokea sana kwa watu wanene kupita kiasi.
Katika aina hii mwili hutumia kidogo au kushindwa kabisa kutumia insulini iliyotengenezwa na kongosho. Kutoitambua insulini kufanywako na seli za mwili (insulin resistance) husababisha mwili kutengeneza insulini nyingi zaidi.Takriban asilimia tisini ya wagonjwa wa kisukari huugua aina hii.

Sabau zihusianazo na aina hii ya Kisukari ni pamoja na sababu za kijenetiki.Jinsi ambavyo sababu za zinachangia hali hii haijulikani lakini jeni (genes) kadhaa zinahusishwa. Hakuna uhusiano na antijeni za chembe hai nyeupe za binadamu.Pia seli za beta, tofauti na kwenye aina ya kwanza, huwa hazijadhurika.

Sababu ya pili ni mwenendo wa maisha.Tabia ya kula kupita kiasi na kuzidi mahitaji ya mwili haswa kwa watu wanene kupita kiasi huchangia katika kupata aina hii ya pili ya kisukari.Unene wa kupita kiasi hufanya insulini kutofanya kazi sawasawa kwa kuongeza ukinzani wa seli katika kuzitambua insulini.

Utapiamlo wa mtoto akiwa tumboni pia umehusishwa na aina hii ya kisukari.Inasemekana kwamba utapiamlo hata ule wa mtoto mchanga aliye chini ya mwaka mmoja huweza kuzidhuru seli za beta zisikue vizuri katika kipindi muhimu cha ukuaji na hivyo kumhatarisha muathirika huyo kupata aina hii ya kisukari baadaye maishani.

Baadhi ya sifa ziambatanazo na aina hii ya kisukari ni pamoja na kuanza baada ya umri wa miaka arobaini, mgonjwa kuwa mnene kupita kiasi, kiwango cha insulini katika damu kuwa kawaida au juu na kiwango cha homoni ya glukagoni kuwa kuwa juu.Pia dalili za ugonjwa huchukua kati ya miezi hadi miaka kuonekana.Dalili hizo ni kuwa na kiu sana, kukojoa mara kwa mara, kuongezeka kwa hamu ya kula, kuchokachoka, kutoona vizuri, mgonjwa kuchelewa kupona baadhi ya magonjwa hasa vidonda na kupungua kwa nguvu za kiume.

(iii) Kisukari kitokanacho na Ujauzito

Aina hii ya kisukari hutokea zaidi kati ya nusu ya pili ya ujauzito yaani kati ya miezi minne na nusu hadi miezi tisa.Ingawa aina hii ya kisukari huisha baada ya kujifungua, wanawake wenye aina hii ya kisukari wana nafasi kubwa kuliko wanawake wengine, ya kupata kisukari kisichotegemea insulini baadaye maishani.

Vigezo hatarishi kwa mtu kupata kisukari:

Kuwa na ndugu (mzazi, kaka au dada) mwenye kisukari

Unene wa kupita kiasi

Umri wa zaidi ya miaka arbaini na mitano (45)

Kuwa shinikizo la juu la damu

Kuwa na kiwango kikubwa cha mafuta (triglycerides) kwenye damu

Kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu (cholesterol) kwenye damu

Kutokufanya mazoezi ya kutosha

Dalili za jumla za ugonjwa wa kisukari ni kama zifuatazo:

Dalili ya kwanza ni Uchovu.Kwa mtu mwenye kisukari, mwili hushindwa au hutumia kwa kiasi kidogo sukari kama nishati mwilini na badala yake hutumia mafuta yaliyoko mwilini.Mchakato huu huugharimu mwili kutumia nishati zaidi na matokeo yake mtu hujisikia mchovu.

Dalili ya pili ni kupungua uzito pasipo sababu.Mtu mwenye kisukari hushindwa kutumia chakula anchokula kutengeneza nishati kwahiyo anaweza kupungua uzito mbali ya kuwa anakula vizuri.Kitendo cha kupoteza sukari na maji kwenye mkojo pamoja na kupungukiwa maji mwilini pia huchangia kupunguza uzito.

Dalili nyingine ni kunywa maji mengi.Mgonjwa wa kisukari huwa na sukari nyingi kwenye damu.Mwili hujaribu kupambana na hali hii kwa kutuma ujumbe kwenye ubongo kupunguza usukari kwa kunywa maji mengi ili pia kulipizia kiasi kilichopotea kutokana na kukojoa sana.

Kukojoa sana ni dalili nyingine ambapo mwili hutumia njia hii katika kujaribu kupunguza kiwango cha ziada cha sukari kwenye damu kupitia kwenye mkojo.

Dalili ya tano ni kula sana.Hali hii hutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha insulini katika mwili.Wingi wa insulini mwilini ni matokeo ya kongosho kuzalisha insulini ili kukabiliana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu.Pia kutokana na seli za mwili kutotaimbua insulini kama tulivyoona kwenye kisukari kisichotegemea insulini,homoni hii huwa nyingi mwilini.

Kuchelewa kupona kwa kidonda ni dalili mojawapo ya kuwepo kwa ugonjwa wa kisukari mwilini.Sukari nyingi katika damu huzuia chembehai nyeupe za damu kutokufanya kazi sawa sawa ya kulinda mwili dhidi ya bakteria na kuondoa seli zilizokufa toka mwilini.

Magonjwa katika njia ya mkojo (urinary tract infection), kwenye sehemu za siri (haswa ya fangasi), kushuka kwa kinga ya mwili kutokana na kisukari pamoja na uwepo wa sukari kwenye viungo ambavyo huchochea bacteria kukua vizuri.

Kutoona vizuri pia huweza kuhusiana na kiwango kikubwa cha sukari katika damu ingawa si lazima kuwepo kwake humaanisha kuwepo kwa ugonjwa wa kisukari.

Jinsi ya kudhibiti Kisukari

Kula mlo kamili mara kwa mara.Usikae na njaa.Mlo uwe na mbogamboga za majani zaidi, mafuta kidogo na upunguzwe vitu vitamu kama pipi, keki,chokoleti n.k

Kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kupunguza madhara zaidi yatokanayo na kisukari kama magonjwa ya moyo, kiharusi (stroke), upofu na vidonda miguuni.

Punguza au acha kabisa kutumia kileo (pombe).Unywaji wa pombe wa kupindukia ni kigezo hatarishi cha kupata kisukari kisichotegemea insulini.

Acha kuvuta sigara (tumbaku) kwani uvutaji huathiri mishipa ya damu na hupelekea kupata magonjwa ya moyo, kiharusi na huhitilafiana na mzunguko wa damu kwenye miguu.

Dhibiti kiwango chako cha sukari kwenye damu kwa kupima mara kwa mara haswa kabla ya mlo na wakati wa kulala. Zingatia matibabu.

Jiunge na kliniki ya watu wenye kisukari iliyo karibu na wewe ili upate elimu na maelezo zaidi kuhusu ugonjwa wa kisukari. Onana na daktari angalau kila baada ya miezi mitatu.


Madhara zaidi yatokanayo na kisukari

Aina zote za kisukari hupelekea kuzidi kwa kiwango cha sukari kwenye damu. Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kwa muda mrefu huharibu macho, figo, mishipa ya fahamu (neva) na mishipa ya damu.

Macho
Mabadiliko yanayotokea kwenye jicho ambayo ni maalum kwa kisukari ni pamoja na mishipa ya damu ya retina kuziba, kuwa migumu na kuvujia kwa damu.Dalili za mwanzo ni kupungua kwa uwezo wa kuona, maumivu kutokana na mwanga na hatimaye kutokuona kabisa (upofu).

Figo
Kutokana na wingi wa sukari katika damu pia huweza kusababisha madhara katika figo na kupelekea kupotea kwa sukari na protini kwenye mkojo.Pia husababisha kusimama kwa figo kufanya kazi (renal failure).

Mishipa ya fahamu (Neva)

Madhara katika mishipa ya fahamu hutokana na kisukari sugu au kisichotibiwa sawasawa.Mgonjwa hulalamika maumivu na wakati mwingine ganzi miguuni.Pia huvimba miguu,hukosa haja ndogo au/na kubwa, kutotoka jasho haswa mikononi na miguuni na hushindwa kusimamisha uume kwa wanaume.Inakadiriwa kuwa takriban asilimia hamsini ya wanaume wanaougua kisukari wanashindwa kwa kiasi fulani kusimamisha uume.


Mishipa ya damu

Sukari nyingi katika damu huathiri mishipa ya damu na hivyo kupelekea kupungua kwa hisia.Pamoja na kupungua kwa damu ifikayo miguuni husababisha kuumia kirahisi kwa dole gumba na unyayo ambako hupelekea kidonda. Kidonda cha mguu huweza kupelekea kukatwa kwa mguu.



Kupungua kwa sukari katika damu

Endapo kutakua na insulini nyingi mwilini na sukari kidogo katika damu, huweza kupelekea kushuka chini ya kiwango cha kawaida kwa sukari katika damu.Hali hii pia huweza kusababishwa na kuzidisha kiwango kitakiwacho cha insulini kwa ajili ya matibabu. Dalili ya mwanzo huwa ni njaa, ikifuatiwa na kizunguzungu, kutokwa jasho, moyo kwenda mbio, kuchanganyikiwa na kisha kupoteza fahamu.

Uchunguzi na Matibabu

Kiwango cha sukari katika damu ndicho kigezo pekee cha kugundua iwapo mtu ana kisukari. Sindano huchomwa kwenye kidole na damu huwekwa kwenye utepe maalum (strip) ambao hupitishwa kwenye mashine iwezayo kugundua kiwango cha sukari katiaka damu (random blood glucose).Njia hii huweza kugundua kwa haraka kiwango cha sukari katika damu ingawa si kipimo makini sana.

Vinginevyo mgonjwa hutakiwa kutokula kitu (kufunga) usiku kucha, kwa angalau masaa nane (8) kabla ya kutolewa damu na kupimwa kiwango cha sukari kwenye damu (fasting blood glucose)
Kipimo kingine ambacho sio maalum sana lakini husaidia kuthibitisha uwepo wa kisukari ni kipimo cha mkojo kuchunguza iwapo kuna sukari (glycosuria) au protini (proteinuria).

Matibabu
Kwa kisukari kitegemeacho insulini, tiba yake ni lazima kupata insulini (sindano)kila siku.
Kwa kisukari kisichotegemea insulini, mazoezi, mlo kamili usio na sukari wala mafuta kwa wingi, mazoezi na madawa (haswa ya kumeza) huweza kukidhibiti.

Ni vizuri kumuona daktari iwapo una dalili zilizotajwa hapo juu kwa ushauri zaidi na epuka kutumia dawa bila ushauri wa daktari.
MWISHIO
______________________________________

0 maoni:

Chapisha Maoni