Siku moja baada ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Simba na kutolewa taarifa kuwa mwanachama wa klabu hiyo ambaye anatajwa kutaka kuwekeza, Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises, Mohammed Dewji “MO” amekuwa akizungumza katika vyombo vya habari na hajafikisha maombi yoyote mbele ya uonngozi huo.
Kufuatia taarifaa hiyo ya uongozi, Mohammed Dewji “MO” ametoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo na kusema si sahihi kuwa hajawahi kukutana na viongozi wa Simba akiwepo Rais wa klabu, Evans Aveva.
“Nilikuwa nafatilia kwa makini mkutano lakini kulikuwa kunatolewa hoja za upotoshaji kuwa viongozi wanasema nimekuwa ninatangaza tu kwenye vyombo vya habari na wao hawajapokea maombi yoyote kutoka kwangu,
“Nimeshakutana na Rais wa Simba, Evans Aveva zaidi ya mara tatu kujadili hilo jambo, ameshakuja ofisini kwangu na wajumbe wa bodi na Kabour zaidi ya mara tatu, si kweli kuwa nazungumza katika vyombo vya habari hili jambo wanalijua,” alisema MO.
Wakati huohuo, MO amesema tayari ametuma barua kwa uongozi wa Simba kuomba kuwekeza baada ya Rais wa Simba, Evans Aveva kusema kuwa wameridhia kufanya mabadiliko.
Aidha MO amewashukuru wanachama wa Simba kwa kuonyesha kukubaliana na mipango yake ambayo amepanga kuifanyia klabu hiyo pindi atakapopata nafasi ya kununua hisa za asilimia 51 kwa kiasi cha fedha cha Bilioni 20.
“Niwashukuru sana wanachama wa Simba kwa kuwa pamoja na mimi na mimi niwaahidi nitawapigania ili kuisaidia timu yetu na kama tukifankiwatutawapatia hisa bure wanachama ambao wamekuwa wakiipigania Simba,” alisema MO.