Postedy by Esta Malibiche On August 17.2016 in News
MKUU wa wilaya ya Kilolo, Asia Abdalla
amezindua wodi ya wazazi iliyojengwa katika Zahanati ya kijiji cha Kiwalamo
wilayani humo huku akiahidi kuchangia toka mfukoni mwake harakati za wananchi
wa kijiji hicho wanaotaka Zahanati hiyo iwe kituo cha afya.
Wodi hiyo yenye uwezo wa kuchukua vitanda
16 vya kupumzisha wajawazito wakati wakisubiri kujifungua imejengwa kwa msaada
wa kampuni ya New Forest, wawekezaji wenye mashamba ya miti yenye ukubwa wa
ekari 12,000 wilayani humo.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa wodi hiyo,
Afisa Mahusiano na Maendeleo ya Jamii wa kampuni hiyo, Robert Nyachia alisema
imejengwa kwa Sh Milioni 49.7 ambazo kati yake Sh Milioni 44.7 ni mchango wa
kampuni yao na Sh Milioni 5 ni mchango wa wananchi.
Nyachia alisema New Forest imechangia
ujenzi huo huku ikitambua umuhimu wa upatikanji wa huduma za afya kwa wote kama
inavyosisitizwa katika Mipango ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs).
Katika kuhakikisha inaanza kutoa huduma
zake, Kaimu Mganga wa Wilaya ya Kilolo, Dk Ibrahim Kisaka alisema halmashauri
ya wilaya hiyo imetumia Sh Milioni 4 kuwezesha wodi hiyo kuwa na baadhi ya
vifaa tiba na dawa muhimu.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Ebineda
William alisema; “kujengwa kwa wodi hiyo ni mkombizi kwao kwani wazazi wengi
tulikuwa tunalazimika kutumia gharama kubwa kufuata huduma za uzazi zinazokosekana
katika zahanati hii katika kituo cha afya Bomalang’ombe au mjini Iringa.”
Akizundua wodi hiyo, DC Abdalla alisema
itasaidia kupunguza au kumaliza tatizo la baadhi ya wajawazito kujifungulia
majumbani au mbali na kijiji hicho kwasababu ya kukosekana kwa huduma hiyo.
“Nawaagiza viongozi wa serikali katika
kijiji hiki na vijiji jirani kuwahamasisha wajawazito kuja hapa kupata huduma
ya kliniki na zingine zitakazotolewa katika wodi hii, tukilenga kuzuia vifo vya
mama na mtoto kwasababu ya ukosefu wa huduma,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya aliyepokelewa na
wananchi ambao baadhi yao walikuwa na mabango yanayotaka Zahanati hiyo
iboreshwe ili iwe kituo cha afya alisema; “nimesikia ombi lenu la kuwa na
huduma bora kabisa za afya, inawezekana mkawa na kituo cha afya lakini ni
lazima mkidhi vigezo vyake vyote.”
Alisema yeye binafsi yupo tayari kutoa
sehemu ya mshahara wake kuchangia harakati hizo endapo wananchi wa kijiji hicho
watakuwa tayari kuchangia ujenzi wa majengo mengine muhimu yatakayoifanya
Zahanati hiyo iwe na sifa ya kuwa kituo cha afya.
Wakimjibu mkuu wa wilaya huyo, wananchi
waliojitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa wodi hiyo walisema wapo tayari
kuchangia ujenzi wa majengo ya ziada na mahitaji mengine yatakayowawezesha
kuifanya zahanati yao iwe na hadhi ya kituo cha afya.
Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Hellen
Chissanga alitaja vigezo mbalimbali muhimu kwa ajili ya uanzishaji wa kituo cha
afya ikiwa ni pamoja na kuwa na chumba cha upasuaji.
0 maoni:
Chapisha Maoni