Mshiriki
Mkuu wa Shindano la Kanumba Star Search, Florence Mutegoa (Mama
Kanumba) amezindua shindano la kusaka vipaji vya waigizaji watakaoigiza
filamu itakayoenzi maisha ya Marehemu Steven Kanumba.
Uzinduzi
huo umefanywa leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) ambapo Mshiriki Mkuu wa Shindano hilo ametoa rai kwa wananchi
kujitokeza kwa wingi kudhamini shindano hilo litakaloibua vipaji vipya
vya uigizaji.
“Tunatambua
thamani ya maigizo ndio sababu tumeamua kuanzisha shindano hili ili
kuibua vipaji vilivyojificha, hivyo tunawakaribisha wananchi wote wenye
uwezo wa kuigiza waje washiriki kwenye mashindano yetu pia tunaomba
wadhamini kujitokeza zaidi ili watusaidie kufanikisha shindano hili”,
alisema Mutegoa.
Mutegoa
amefafanua kuwa shindano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Kampuni
ya Kanumba the Great Film na Kampuni ya AM Arts Promotion ambapo hadi
sasa shindano hilo lina mdhamini mmoja kutoka Kampuni ya simu za mkononi
za KZG – Tanzania.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AM Arts Promotion, James
Mwombeki amesema kuwa marehemu Kanumba alikuwa na mchango mkubwa katika
kuitangaza nchi kimataifa pamoja na kuibua vipaji vya wasanii wa maigizo
hivyo hatuna budi kumuenzi kwa kuiendeleza Sanaa ya uigizaji.
“Sisi
kama AM Arts Promotion tumeamua kushirikiana kwa pamoja na Mama Kanumba
kufanya shindano hili kwa nia ya kuendeleza tasnia ya filamu nchini
kama vile marehemu Kanumba alivyokua akijitahidi kuwapa fursa ya
uigizaji watu wa kila rika”, alisema Mwombeki.
Naye,
Msanii wa filamu, Mayasa Mrisho amewasisitiza wananchi kushiriki kwa
wingi kwenye mashindano hayo kwani Sanaa ya uigizaji ni njia mojawapo ya
kujipatia kipato na kuinua maisha ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Aidha,
Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu za Mkononi za KZG – Tanzania, Raymond
Kalikawe amesema kuwa wamekubali kuwa wadhamini wa shindano hilo kwa
kuwa ukuzaji wa vipaji vya wasanii wa maigizo ni jambo muhimu pia
amewaomba wadhamini wengine kujitokeza zaidi kusaidia shindano hilo.
Shindano
hilo linatarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu, litaanzia Mikoa ya
Kanda ya ziwa na baadae kuendelea katika Mikoa mingine.Washindi
wataigiza filamu ya kumuenzi marehemu Kanumba itakayojulikana kama
“Maisha ya Kanumba.
0 maoni:
Chapisha Maoni