Postedy by Esta Malibiche on August 10.2016
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya
TEHAMA, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Arnold Mathoyo
akieleza utaratibu wa mafunzo ya TEHAMA kwa washiriki wanaosimamia
miradi ya TEHAMA chini ya Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP)
Tanzania katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa,
Dodoma.(James Katubuka Mwanamyoto)
Washiriki wa mafunzo kuhusu TEHAMA
wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi (hayupo pichani).
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi i
akifungua mafunzo kwa wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) wanaosimamia miradi chini ya Mradi wa Miundombinu ya
Mawasiliano (RCIP) Tanzania katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na
Nyaraka za Taifa, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi
akisisitiza jambo wakati akifungua mafunzo kwa wataalam wa TEHAMA
wanaosimamia miradi chini ya Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP)
Tanzania katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa,
Dodoma.
………………………………………………………………………………………
Usimamizi na utekelezaji wa Serikali Mtandao unahitaji Rasilimaliwatu yenye weledi mkubwa wa kusimamia maeneo ya msingi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi
alisema hayo mkoani Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa
miradi mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
inayotekelezwa chini ya Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano (RCIP)
Tanzania.
“ Rasilimaliwatu katika eneo hili
inahitaji kupewa mafunzo na kuendelezwa katika nyanja muhimu za
usimamizi wa TEHAMA na pia kuwa na uwezo na uelewa wa mifumo na taratibu
za utendaji kazi katika Taasisi za Umma” Bi. Mlawi alisema.
Bi. Mlawi alifafanua kuwa, mafunzo
hayo ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la Serikali la kuwajengea uwezo
wataalam wake ili kuboresha utekelezaji wa miradi ya Serikali Mtandao
yenye lengo la kuziwezesha Taasisi za Umma kutoa huduma bora kwa
Wananchi.
Aliongeza kuwa, mafunzo hayo
yamelenga kuongeza uwezo kwa wataalam wa Serikali hususani katika
Ununuzi na usimamizi wa utekelezaji wa mifumo na mitandao mbalimbali ya
TEHAMA inayowekwa katika Taasisi za Serikali ili kuboresha utendaji
kazi na utoaji wa huduma kwa Umma.
Bi. Mlawi aliainisha kuwa uteuzi
wa washiriki wa mafunzo hayo umezingatia ushiriki katika utekelezaji wa
miradi ya RCIP na matokeo ya utafiti wa mahitaji ya mafunzo kwa maafisa
TEHAMA wa Taasisi za Serikali, uliofanywa na Wakala ya Serikali Mtandao
(eGA) mwezi Septemba, 2015.
Alisisitiza kuwa, kila mshiriki
atajengewa uwezo wa kiufundi kulingana na mahitaji halisi katika eneo au
maeneo ya kusimamia na kutengeneza mifumo ya TEHAMA.
Naibu Katibu Mkuu huyo Bi. Mlawi,
alielekeza washiriki wa mafunzo hayo wahakikishe ujuzi watakaoupata
unawafikia wale ambao hawakubahatika kuchaguliwa kwa sababu idadi ya
washiriki walioteuliwa kuhudhuria mafunzo ni ndogo ikilinganishwa ya
idadi kubwa ya Maafisa TEHAMA waliopo katika Taasisi za Serikali ili
kwa pamoja washirikiane kubuni mifumo ya TEHAMA yenye kuboresha
utendaji kazi na utoaji huduma kwa umma.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina jukumu la kuratibu na kusimamia
utekelezaji wa miradi ya RCIP eneo la Mifumo ya Serikali Mtandao “e-Government Applications”
ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA (ya Kimkakati na ya Kisekta)
inaendelea kuwekwa na kutekelezwa katika Taasisi walizotoka washiriki wa
mafunzo.
Mifumo hiyo ni Mfumo wa Wakala ya Usajili, Vizazi na Vifo (Birth and Death Registration System) kupitia Wakala ya RITA; Mfumo wa Taarifa za Biashara (National Business Portal) kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, Mfumo wa Taarifa za Kitabibu (Telemedicine system) kupitia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mfumo wa Taarifa za Ununuzi (e-Procurement system) kupitia Mamlaka ya Uthibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Bohari ya Dawa (MSD), Mradi wa “electronic Records” kupitia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa na; Mradi wa “electronic Office” kupitia Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).
Mafunzo hayo yatatolewa kwa Maafisa, Wasimamizi wa miradi
62; Wakuu wa Vitengo vya TEHAMA 15 na Maafisa Ugavi 50 kutoka kwenye
Taasisi mbalimbali za Serikali na yatafanyika kwa awamu 5 katika ukumbi
wa Mikutano wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Dodoma.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais-UTUMISHI
0 maoni:
Chapisha Maoni