Rubani Kevin Chibole wa Shirika la ndege la Precision baada ya kutua kwenye kiwanja cha ndege cha Dodoma hivi karibuni.
Ndege ya shirika la ndege ya
Precision baada ya kutua kwenye kiwanja cha ndege cha Dodoma baada ya
kurefushwa kwa barabara ya kuruka na kutua kutoka kilometa 2 hadi
kufikia kilometa 2.5.
………………………………………………………………………..
RUBANI Kevin Chibole wa shirika la
ndege la Precision, amesema atawashawishi waajiri wake, kuanza safari
za kutoka Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA)
kilichopo jijini Dar es Salaam na kwenda kiwanja cha ndege cha Dodoma,
kwani sasa barabara yake ya kutua na kuruka kwa ndege imerefushwa zaidi.
Chibole, aliyerusha ndege ATR 72
5H PWA, amesema awali walishindwa kufanya safari kwenye kiwanja cha
ndege cha Dodoma, kutokana na barabara yake ya kutua na kuruka ndege
kuwa fupi kwa urefu wa kilometa 2, lakini sasa imerefushwa hadi kufika
kilometa 2.5, itakayoruhusu ndege kubwa kutua na kuruka bila tatizo.
“Hii runway (barabara ya kutua na
kuruka ndege) ni nzuri haina mabondebonde, hivyo sasa umefika wakati
muafaka kuwaeleza wamiliki wa ndege hii, tuanze safari ya hapa Dodoma
kwa kutokea JNIA,” alisema Chibole.
Naye Waziri wa Ofisi ya Rais
Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe, Harun Ally Suleiman aliyekuwa miongoni mwa
abiria 37 waliokuwa wamepanda ndege hiyo iliyotoka kwenye Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Amani Abeid Karume (AAKIA) Zanzibar na kutua
JNIA na baadaye kuanza safari ya Dodoma, alisema hakuwahi kwenda Dodoma
kwa ndege kubwa, na safari hiyo imekuwa ya kwanza kwake.
“Tunaishukuru Serikali ya Rais
Magufuli, kwani tunaona kunaujenzi unaoendelea hapa na hata tumeambiwa
kuwa hii barabara tuliyotua na ndege ya Precision imeongezwa urefu na
ndio maana ndege hii ikaweza kutua, tunashukuru sana kwa hili,” alisema
Mhe. Harun.
Amesema miundombinu ya usafiri
ikiboreshwa itasaidia eneo husika kukuza uchumi wake, ambapo sasa Dodoma
itakuwa juu kiuchumi kwa kuwa tayari wafanyabiashara watatumia zaidi
usafiri wa ndege kwa kuwa ni wa haraka na uhakika.
Pia abiria mwingine aliyesafiri
kwa ndege hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe Juma alisema kuwa awali wajumbe
wa mkutano mkuu wa Chama tawala kutoka Zanzibar, walikuwa wakitumia
zaidi usafiri kwa barabara, kutokana Dar es Salaam hadi Dodoma kutokana
na kutokuwa na ndege kubwa ya kutosheleza wajumbe wote kwa pamoja, ila
kurefushwa kwa barabara ya kutua na kuruka imekuwa faraja na kufanya
safari kuwa fupi na haraka.
“Naona namna gani Serikali ya
Awamu ya Tano, inavyotekeleza kwa kasi ahadi zake, na hii ni mojawapo ya
upanuzi wa kiwanja, ambapo kitaleta tija kwa wakazi wa hapa na nchi
nzima kwa ujumla,” alisema Mhe. Riziki.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi George Sambali alisema
kutua vizuri kwa ndege ya shirika la ndege la Precision ATR 72 5H PWA
kutachochea ongezeko la ndege kubwa zaidi zenye uwezo wa kubeba abiria
kuanzia 50 hadi 90 kutua kwenye kiwanja cha ndege cha Dodoma.
“Tuliambiwa na Mh. Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akiweka
jiwe la msingi la ukarabati na upanuzi wa kiwanja hiki cha Dodoma, kuwa
hapa patakuwa ni kitovu cha shughuli mbalimbali hivyo zitaanza kuja
ndege kubwa zikiwemo za ATCL zinazotarajiwa kuwasili nchini Septemba
2016, hivyo ni matumaini yangu kuwa hata bei ya safari itashuka maana
zitakuwa nyingi,” alisema Mhandisi Sambali.
Wakati wa uwekaji wa jiwe la
msingi la mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Dodoma,
uliofanyika hivi karibuni Mh. Waziri Mkuu, Kassim M. Majaliwa alisema
kutokana na kurefushwa kwa barabara hiyo, sasa kiwanja hiki kitakuwa na
uwezo wa kupokea ndege kubwa za ATCL, Precision na Fastjet, na gharama
itapungua.
Kazi ya ukarabati na upanuzi huo
inayosimamiwa na timu ya Wahandisi wazawa wanaoogozwa na Mhandisi Mbila
Mdemu kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), huku
mkandarasi akiwa ni Kampuni ya China Henan International Cooperation
(CHICO) Group Co. Ltd kutoka Jamhuri ya watu wa China. Tayari ujenzi
umekamilika kwa asilimia 65, ambapo hivi karibuni Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe, Prof. Makame Mbarawa, aliyetembelea kuona
maendeleo ya kazi hiyo iliyoanza siku 45 zilizopita.
“Mradi huu umetupa mfano kama
tukijipanga vizuri hata kwenye miradi mingine tunaweza kutekeleza kwa
haraka na ubora unaotakiwa, kwa upande wetu kama Serikali tutahakikisha
kiwanja hiki kinakamilika haraka ili kuruhusu ndege kubwa kuanza kutua”,
amesisitiza Waziri Mbarawa.
Aidha ameongeza kuwa kukamilika
kwa ujenzi wa uwanja huo utakuwa chachu kwa Shirika la Ndege Tanzania
(ATCL) kuwaunganisha watanzania kwa kutoa huduma za usafiri anga
katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa
uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa
upanuzi huo Mdemu amesema mpaka sasa mita 2450 zimekamilika kwa kuweka
tabaka la kwanza lami katika eneo la kuruka na kutua ndege.
“Kasi ya ujenzi wa kiwanja hiki
inaendelea vizuri kwa kushirikiana na mkandarasi wa kampuni ya CHICO na
kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati kwa kuzingatia viwango na
ubora unaotakiwa”, amesema Mhandisi Mdemu.
Upanuzi wa uwanja wa ndege wa
Dodoma unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa Km
2.5, barabara za viungio na maegesho ya ndege.
0 maoni:
Chapisha Maoni