Alhamisi, 4 Agosti 2016

Mtaturu:Hakuna demokrasia yoyote duniani inayohubiri wananchi kutoshiriki shughuli za maendeleo

 
Na Mathias Canal, Singida
 
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Mh. Miraji Jumanne Mtaturu  amsema hakuna demokrasia yoyote duniani inayohubiri wananchi kutoshiriki shughuli za maendeleo hivyo mwananchi anapaswa
kushirikishwa katika kuchagua viongozi wake, kukaa na viongozi wake kupanga miradi ya maendeleo kama vile kuchangia ujenzi wa shule, zahanati na maabara na maendeleo mengine.
Ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo kwa kutumia nguvu na akili katika kukamilisha na kumiliki miradi ya kijamii
ni njia mojawapo itakayowafanya wananchi kuwa na uchungu na mali pamoja na maendeleo  katika jamii husika.
 
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa kumekuwa na matumizi mabaya ya demokrasia katika Wilaya hiyo hususani katika shughuli za kijamii kama vile kuchangia ujenzi wa maabara jambo lililopelekea Wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika ujenzi wa maabara kwa ajili ya shule za sekondari zilizopo katika Wilaya ya Ikungi.
“Wataalamu wa Sayansi na viongozi mashuhuri wamewahi kusema Demokrasia bila maendeleo sio demokrasia, Hayati Mwalimu julius Kambarage Nyerere na Profesa Issa Shivji waliwahi kuandika kuwa demokrasia ya kweli ni ile inayowasaidia wananchi kutoka katika hali moja kwenda kwenye hali nyingine ambayo ni bora zaidi kuliko ile waliyo nayo, hivyo tukiongelea kuwashirikisha wananchi katika mipango na mikakati ya kuondokana na umasiki na si vinginevyo” Alisema Mtaturu
 
Dc Mtaturu amesema kuwa kuwa mwenyekiti wa Kijiji kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), CHADEMA, ACT WAZALENDO, CUF au chama chochote hapaswi kuongoza wananchi kwa matakwa yake binafsi bali ni lazima kufuata taratibu, kanuni, sheria na taratibu zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yao.
 
Ameyasema hayo wakati wa kikao cha kazi kati ya Mkuu waWilaya Wakuu wa idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Weneyeviti wa Vijiji na
Watendaji wa Kata na Vijiji katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.  
 
Amewaelekeza wenyeviti wa Vijiji kuwa majukumu  yao ni kuongoza vikao vya Halmashauri ya Kijiji na kuongoza mkutano mkuu wa Kijiji sio kuuza ardhi ya kijiji kiholela, Kumnyang’anya mtu ardhi au kupiga faini yoyote wanayojisikia na ndio maana kunakuwa na watendaji wa Vijiji ambao ni wataalamu hivyo wana majukumu muhimu katika kuwashauri wenyeviti wa Vijiji.
 
Dc Mtaturu pia amewataka viongozi hao kutambua kuwa uchaguzi ulimalizika Octoba mwaka jana na chama kilichoshika dola ni Chama Cha Mapinduzi
(CCM) hivyo kutokana na uchaguzi huo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipewa ridhaa ya kuongoza Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano 2015-2020 hivyo ilani inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo kwa vile kila kiongozi wa Kijiji yupo ndani ya serikali anapaswa kutelekeza ilani ya CCM kwani huo ni utaratibu wa vyama vinavyoshinda popote dunia.
 
Baadhi ya watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, na baadhi ya watendaji wa Vijiji Wilayani Ikungi hawajawahi kupatiwa mafunzo ya
muongozo wa kiutendaji hali iliyopelekea baadhi yao kutotimiza wajibu wao na wengine kufanya kazi nje ya mipaka yao.
 
“ Kupitia kikao/mafunzo haya Uonevu wowote, kosa lolote, matumizi mabaya ya madaraka yatakayofanywa aidha na Mtendaji wa Kata,
Mwenyekiti wa Kijiji, Mtendaji wa Kijiji sitalifumbia macho nitakuchukulia hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni, tulizowekeana kama serikali” Alisema Mtaturu
 
Sambama na hayo Dc Mtaturu amewasihi viongozi hao kuwaunga mkono askari polisi katika kuimarisha ulinzi na usalama kwani bila usalama na amani katika jamii inayotuzunguka hakuwezi kuwa na maendeleo.

0 maoni:

Chapisha Maoni