DEREVA  wa basi la kampuni ya City  Boys T.531 DCE Boniface Douglas Mwakalukwa (37) mkazi wa jijini Dar-es-salaam, ambaye alitoroka baada ya basi alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na basi jingine la kampuni ya City Boys, amejisalimisha mbele ya polisi na kufikishwa mahakamani.
Mtuhumiwa Mkwakalukwa anatuhimiwa kwa makosa 30 kujibu tuhuma inayomkabili  ya mauaji ya abiria 30 bila kukusudia.
Mtuhumiwa Mwakwalukwa leo ameunganishwa kwenye kesi  iliyosajiliwa na kupewa namba 22/2016.Mtuhumiwa huyo ameunganishwa na dereva mwenzake Jeremia Martin Simpumgwe (34) ambaye mara ya kwanza alipandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini hapa,julai nane mwaka huu.Jeremia ni mkazi wa Kimara Temboni jijini Dar-es-salaam.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu 195 na 198 cha kanuni ya adhabu sura 16 toleo la kwanza kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Mapema mwendesha mashitaka wakili wa serikali Petrida Muta, amedai mbele ya hakimu mkazi mwandamizi Joyce Minde,kuwa mnano Julai nne mwaka huu saa 8.15 mchana huko katika kijiji cha Maweni wilaya ya Manyoni,washitakiwa wote wakiwa waajiriwa wa kampuni ya mabasi ya City Boys,walisababisha mabasi waliyokuwa wakiyaendesha kugongana uso kwa uso,na kusabaisha vifo vya abiria 30.
Washitakiwa hao hawakujibu chochote, kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Muta alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, na akaiomba mahakama hiyo isiwape dhamana washitakiwa,kwa madai kwamba mazingira kwa sasa hayaruhusu washitakiwa kuwa nje.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 4 mwaka huu, itakapotajwa tena.
Imeandikwa na Nathaniel Limu, Singida
City Boys Bus Drivers
Madereva wawili wa mabasi ya kampuni ya City Boys (mmoja ni aliyeficha uso kwa bahasha ya kaki) wanaotuhumiwa kwa makosa 30 ya mauaji abiria bila kukusudia, wakiwa na wenzao wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali, wakisindikizwa mahakamani mapema leo asubuhi.(Picha na Nathaniel Limu).