Baadhi
ya wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar wakifuatilia
ufungaji wa mafunzo elekezi yaliyofanyika katika Chuo chao Chwaka Mkoa
Kusini Unguja.
Mratibu
wa mafunzo elekezi ya wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar
Said Mohd Khamis akieleza lengo la Chuo kuanzisha mpango wa wanafunzi
kufanya mazoezi ya vitendo katika taasisi za kijamii.
Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na
Watoto Mauwa Makame Rajab akifunga mafunzo elekezi ya wanafunzi wa Chuo
cha Uongozi wa Fedha Zanzibar watakaoshiriki mazoezi ya vitendo katika
vikundi vya kijamii (kushoto) Mkurugenzi wa Vyama vya Ushirika Zanzibar
Khamis Simba na (kulia) Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt. Iddi.
…………………………………………………………………………………….
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
CHUO cha Uongozi wa Fedha
Zanzibar (ZIFA) kimeanzisha mpango wa kuwapeleka wanafunzi wa Chuo hicho
kufanya mazoezi ya vitendo katika vikundi vya Kijamii (SACCOS) kuanzia
mwaka huu.
Uamuzi huo unafuatia muongozo
uliotolewa na Baraza la Chuo baada ya kubaini kuwa wanafunzi wengi
wanapokuwa katika mazoezi ya vitendo katika Mawizara, Maidara na Taasisi
za Umma wanakaa maofisini bila ya kufanya kazi yoyote na kutofaidika na
mazoezi yao.
Jumla ya wanafunzi 130 wa mwaka
wa pili shahada ya kwanza wanaosoma fani ya Uhasibu, Manunuzi na Tehama
wataanza mazoezi ya vitendo katika SACCOS za Unguja na Pemba baada ya
kupatiwa mafunzo elekezi ya siku tatu yaliyotolewa na Idara ya Vyama vya
Ushirika kwa kushirikiana na ZIFA.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo,
Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa
Fedha Maalim Said Mohd Khamis alisema lengo la mpango huo ni kuwawezesha
wanafunzi kutoa elimu kwa jamii baada ya masomo yao.
Amesema vyama vingi vya ushirika
vinakabiliwa na matatizo hasa katika masuala ya uhasibu, manunuzi na
matumizi ya Tehama hivyo wanafunzi wao watakwenda kusaidia katika kutoa
elimu kwa wanachama wa vikundi hivyo.
‘’Wanafunzi wetu watakwenda
kufundisha matumizi ya Teknolojia ya kisasa, utaratibu mzuri wa manunuzi
na masuala ya uhasibu”, alisisitiza Maalim Said.
Ameongeza kuwa mtazamo wa Chuo ni
kutoa huduma na fursa zinazopatikana chuoni hapo kwa jamii ili
kuisaidia Serikali katika juhudi zake za kuwapunguzia wananchi hali
ngumu ya maisha.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Mauwa Makame Rajab
amewaeleza wanafunzi hao kuwa baadhi ya SACCOS wanachama wake hawana
taaluma kubwa katika masuala ya ushirika hivyo mchango wao utasaidia
sana katika kuviimarisha vikundi hivyo.
Amewataka vijana hao kuitumia
elimu waliyonayo na fursa waliyopata ya kufanyakazi katika vikundi vya
kijamii vijijini kujiajiri kwa kuanzisha SACCOS ama kuongoza ziliopo
katika kukabiliana na tatizo kubwa la ajira liliopo.
Amewashauri wanafunzi hao kuwa
mabalozi wazuri katika sehemu watakazokwenda kupinga vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia vinavyozidi kuongozeka katika maeneo mbali
mbali ya Unguja na Pemba.
Aidha amevishauri vyuo vyengine
viliopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla kuiga mfano ulioonyeshwa na ZIFA
kuwapeleka wanafunzi wao kufanya mazoezi ya vitendo katika vikundi vya
kijamii kusaidia masuala mbali mbali ikiwemo sheria, uongozi demokrasia
ndani ya vikundi vyao.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa
Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar amesema wameupokea mpango wa Chuo
kwenda kusaidia vikundi vya ushirika vijijini kwa moyo safi na ameahidi
watatoa mchango mkubwa.
Amesema wanauchukulia mpango huo
kama ni majaribio kwao na watajitahidi kuweka mazingira mazuri na kuwa
mfano wa kuigwa na wanafunzi wenzao watakaofuata hapo baadae.
0 maoni:
Chapisha Maoni