Halmashauri ya wilaya ya Manyoni (kabla ya kutengwa Itigi kuwa halmashauri),imeongoza mkoani hapa, kwa kuwa na kaya 37,569 ambazo hazina vyoo,sawa na asilimia 61 ya kaya 61,723 za halmashauri hiyo.
Hayo yamesemwa na mganga mkuu wa mkoa wa Singida, Dk.John Mwombeki, wakati akitoa taarifa ya huduma mbalimbali za afya mkoani hapa.
Alisema halmashauri hiyo ya Manyoni, ina kaya 9,253 zenye vyoo bora sawa na asilimia 15 na kaya zingine 15,008 zina vyoo vya muda sawa na asilimia 24.
Dk. Mwombeki alisema halmashauri ya wilaya ya Manyoni inafuatiwa kwa mbali na halmashauri ya wilaya ya Singida yenye kaya 5,129 ambazo hazina kabisa vyoo sawa na asilimia 12 ya kaya 42,172.
“Halmashauri ya wilaya ya Singida ina kaya 8,567 zenye vyoo bora sawa na asilimia 20,wakati kaya 28,583 zina vyoo vya muda sawa na asilimia 68,” alisema.
Aidha, mganga mkuu huyo, alisema halmashauri ya wilaya ya Iramba ina kaya 4,882 sawa na asilimia 10 ya kaya 51,022 ambazo hazina vyoo. Kaya 13,498 sawa na asilimia 26 zina vyoo bora na zingine 32,642 zina vyoo vya muda sawa na asilimia 64.
Kwa upande wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Dk.Mwombeki alisema kuwa ina kaya 4,411 ambazo hazina vyoo sawa na asilimia 8 ya kaya 55,829 za halmashauri hiyo changa.
“Hata hivyo, halmashauri ya wilaya ya Ikungi, ina kaya 11,280 zenye vyoo bora sawa na asilimia 20, wakati kaya 40,187 sawa na asilimia 72 zina vyoo vya muda.Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,ina kaya 2,098 sawa na asilimia sita (6) ambazo hazina vyoo,kati ya kaya 34,966,” alisema.
“Mkalama pia ina kaya 11,541 zenye vyoo bora sawa na asilimia 33, wakati kaya 21,359 sawa na asilimia 61 zina vyoo vya muda. Halmashauri ya manispaa ya Singida, yenyewe ina kaya 430 sawa na asilimia moja ya kaya 32,389 ambazo hazina vyoo. Pia manispaa hiyo ina kaya 20,623 sawa na asilimia 69 zenye vyoo bora na kaya 11,336 sawa na asilimia 35, zina vyoo vya muda,” alisema Dk.Mwombeki.
Alisema kwa ujumla, mkoa wa Singida wenye kaya 278,101, kaya 53,974 sawa na asilimia 19, hazina vyoo, kaya 74,760 sawa na asilimia 27 zina vyoo bora na kaya 149,115 sawa na asilimia 54 zina vyoo vya muda.
“Natoa wito kwa mamlaka zinazohusika,ziongeze juhudi kuhakikisha kila kaya inamiliki choo bora na kinatumika ipasavyo,” alisema.
Wakati huo huo, Dk.Mwombeki amesema kuwa pamoja na halmashauri ya wilaya ya Manyoni kuongoza kwa kaya nyingi kutokuwa na vyoo ni halmashauri pekee mkoani hapa, ambayo haikukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu ambao ulikumba wilaya zingine zote kuanzia Septemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu.

Na Nathaniel Limu, Singida