Licha ya kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini kwa upande mwingine kumekuwa na maumivu kwa Yanga baada ya Chama cha Soka cha Afrika (CAF) kuikuta na makosa iliyoyafanya katika mchezo dhidi ya Sagrad Esperanca ya Angola.
Kamati ya Nidhamu ya CAF iliyofanya kikao chake makao makuu ya CAF yaliyopo Cairo, Misri iliikuta Yanga na kosa la kumsonga refa wa mchezo huo pamoja na kupoteza muda baada ya Esperanca kupiga penati na hivyo kuipiga Yanga faini ya Dola 10,000 za Kimarekani.
Aidha CAF imewapunguzia Yanga adhabu kwa kuitaka kulipa Dola 5,000 ambazo zinakaribia kufika Milioni 12 kwa pesa ya Tanzania lakini kuwapa masharti kuwa wasirudie kosa hilo.
Katika mchezo huo uliochezwa Mei, 18, Yanga iliibuka na ushindi wa goli 2-1.
Aidha CAF imeipiga faini ya Dola 10,000 Mo Bejaia ya Algeria kwa kosa la mashabiki wake wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kurusha fataki katika mchezo wake na Yanga, mchezo huo ulimalizika kwa Yanga kukubali kichapo cha goli moja kwa bila.