Kambi
ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo Mkoa wa Kigoma
imewatengea eneo maalumu la kuishi watu wenye ulemavu wa ngozi ili
kulinda usalama wa maisha yao.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Kambi hiyo, Peter Buluku alipokuwa akiongea na
mwandishi wa habari hii juu ya maisha halisi ya wakimbizi hao wanaoishi
katika kambi hiyo wakitokea nchini Burundi.
Buluku
amesema kuwa katika kambi hiyo kuna baadhi ya wakimbizi wanaojihusisha
na vitendo vinavyohatarisha usalama wa wakimbizi wenzao vikiwemo vya
ubakaji, wizi na kujaribu kuteka watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mkuu
huyo wa kambi amefafanua kuwa mnamo mwezi Aprili mwaka huu, familia
moja yenye mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ilivamiwa na watu wasiojulikana
na kumchukua mtoto huyo lakini kwa bahati nzuri majirani walijitahidi
kupiga kelele hivyo, watuhumiwa waliamua kumtelekeza mtoto huyo na
kukimbilia kusikojulikana.
Mkuu wa Kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo, Mkoa wa Kigoma Bw. Peter Buluku.
“Kutokana
na kujitokeza kwa hali hiyo, Sisi pamoja na Mashirika yasiyo ya
Kiserikali yanayotoa huduma kambini hapa tuliamua kuwatengea eneo
maalumu lililo karibu na kituo cha polisi watu hawa wenye ulemavu wa
ngozi ili wawe na ulinzi wa kutosha hivyo kuishi kwa amani kama binadamu
wengine”, alisema Buluku.
Hadi
sasa kambi hiyo ina jumla ya watu watano wenye ulemavu wa ngozi kutoka
kwenye familia mbili tofauti, Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani
(UNHCR) limehaidi kujenga jengo la kudumu kwa ajili ya watu wenye
ulemavu huo.
Kambi
ya Nduta ilianzishwa rasmi mwaka 1998 na kufungwa mwaka 2009.
Ilifunguliwa kwa mara ya pili mwaka 2015 baada ya kutokea kwa vurugu
nchini Burundi na kusababisha baadhi ya raia wa nchi hiyo kukimbilia
nchini Tanzania, hadi sasa kambi hiyo ina jumla ya wakimbizi 55,320
ambao ni raia wa Burundi.
Imeandikwa na Jacquiline Mrisho – MAELEZO Kigoma
0 maoni:
Chapisha Maoni