Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. MAKAME MBARAWA amewataka
wahandisi na makandarasi nchini kujielimisha vya kutosha kuhusu mfumo
mpya wa ujenzi wa barabara wa mikataba inayopima huduma zinazopatikana
kwenye barabara hizo.
Mfumo
huo ambao unaotumiwa na nchi zilizoendelea utawawezesha makandarasi
nchini kujenga barabara kwa mkataba wa muda mrefu wa kupima huduma ya
barabara na mkandarasi atalipwa kulingana na matokeo.
Akifungua
semina ya wadau wa barabara kutoka nchi 19 na taasisi 30 duniani
inaofanyika jijini Arusha Prof. Mbarawa amesema utaratibu huo mpya
utawawezesha makandarasi kujenga barabara za kiwango cha juu zenye ubora
na usalama na kupunguza utaratibu wa ukarabati wa kila wakati
unaogharimu serikali fedha nyingi.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wa pili kushoto
akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC), wa
pili kulia ni katibu mkuu wizara hiyo sekta ya Ujenzi Eng. Joseph
Nyamhanga na wa kwanza kushoto ni mkuu wa mkoa wa Arusha Daudi Felix
Ntibenda.
“Ukijenga
barabara kwa viwango vya juu na ukiisimamia mwenyewe kwa muda mrefu
itapunguza gharama za ukarabati wa kila mwaka zinazotolewa na serikali”
amesema Prof. Mbarawa
Profesa
Mbarawa amekiri uwepo wa changamoto kubwa kwenye ujenzi na ukarabati wa
barabara za wilaya na kusisitiza kwamba barabara nyingi zinajengwa
chini ya kiwango na hazina uwiano na thamani ya fedha zilizotumika.
“Serikali
inajipanga kuanzisha wakala wa barabara za wilaya utakaohakikisha
unafanya kazi kama ilivyo kwa wakala wa barabara kuu na za mikoa ili
kuongeza ufanisi” amesema Prof. Mbarawa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiteta jambo
na Katibu Mkuu Wizara hiyo sekta ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga kabla
ya ufunguzi rasmi wa semina ya wadau wa masuala ya barabara mjini
Arusha.
Profesa
Mbarawa amepongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kwa kazi nzuri ya
kusambaza fedha za ujenzi wa barabara katika halmashauri zote kwa wakati
na kuwataka viongozi wa halmashauri hizo wazitumie fedha hizo kwa kazi
zilizokusudiwa.
“Atakayecheza
na fedha za mfuko wa barabara hatutakuwa na uvumilivu naye, tunataka
fedha hizo zifanye kazi iliyokusudiwa ili adhma ya kufikia uchumi wa
kati ifikapo 2025 kwa kuwa na miundombinu bora ifanikiwe” amefafanua
Prof. Mbarawa.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, sekta ya
ujenzi Eng. JOSEPH NYAMHANGA amesema semina hiyo ya siku tano inawaleta
wataalam wa barabara nchini kujadili changamoto na mafanikio ya mfumo
mpya ya ujenzi wa barabara na mfumo huo utakapoanza utapunguza gharama
za ujenzi na kuwaongezea nguvu makandarasi wazawa.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha Daudi Felix Ntibenda kushoto akijadiliana jambo na
mkuu wa mkoa wa Singida Mathew Mtigumwe kulia walipokutana katika semina
ya wadau wa masuala ya barabara,
Amesema
Tanzania ina takribani ya km 87,481 za mtandao wa barabara ambapo km
35,000 ni barabara kuu na za mikoa, km 52, 581 ni barabara za wilaya
ambapo zote zitanufaika na mfumo huo utakapoanza.
Naye
meneja wa bodi ya mfuko wa barabara Joseph Haule amesema utaratibu huu
mpya utakapoanza nchini utapunguza gharama za ujenzi wa barabara kwa
asilimia 30 na utanufaisha wahandisi na makandarasi wengi nchini
kutokana na sera nzuri ya kuwalinda makandarasi wazawa.
Takribani
wataalam 200 wa masuala ya barabara kutoka nchi za Afrika, Ulaya na
Amerika wanashiriki katika semina hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa
shirikisho la masuala ya barabara Bw. Kiran Kapila lengo likiwa ni
kubadilishana uzoefu katika masuala ya ujenzi wa barabara bora kwa
gharama nafuu.
Imetolewa na kitengo cha habari na mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua
jambo wakati wa ufunguzi wa semina ya wadau wa barabara iliyoanza leo
mjini Arusha.
Wadau
wa masuala ya barabara wakifuatilia kwa makini mijadala katika semina
ya mikataba ya muda mrefu ya kupima huduma itolewayo na barabara na
matokeo yake inayoendelea mjini Arusha.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa katika picha ya
pamoja mara baada ya kufungua rasmi semina ya wadau wa barabara mjini
Arusha.
0 maoni:
Chapisha Maoni