Katibu wa BAKWATA mkoa wa Singida, Alhaj Burhani Mlau, ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuiboresha adhabu (faini ) wanazotozwa madereva kwa makosa ya kukiuka sheria za usalama barabarani, kwa madai faini iliyopo hivi sasa ya shilingi 30,000, imefeli katika kuwaogopesha madereva.
Amesema ajali za barabarani ambazo nyingi zinasababishwa na uzembe, kwa sasa zimekuwa ni wimbo wa kila siku na zinachangia Watanzania wengi kupoteza maisha na mali zao. Kwa hiyo, zinatakiwa zitafutiwe dawa stahiki itakayosaidia kupunguza ajali kwa kiwango cha juu.
“Dereva wa basi la kampuni ya City Boy lililokuwa linatokea Kahama ambalo lilihusika na ajali mbaya iliyotokea Manyoni siku chache zilizopita, alipofika Singida alitozwa faini ya shilingi 30,000 kwa kosa la kuendesha basi kwa mwendo kasi. Lakini baada ya kulipa faini hiyo ndogo, aliendekeza tabia yake ya kuendesha kwa mwendo kasi na mwisho wa siku, alisababisha idadi kubwa ya Watanzania kupoteza maisha yao,” alisema Alhaj Mlau kwa masikitiko makubwa.
Alisema umefika wakati sasa serikali iangalie upya uwezekano wa kutoa sheria ambayo atawaogopesha madereva kwenda kinyume na sheria za usalama barabarani.
“Mapendekezo yangu adhabu kwa madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, wakipatikana na hatia, watozwe faini ya shilingi milioni tatu, wafungwe jela miaka 30 au maisha. Kwa kifupi inatakiwa adhabu kwa watu hawa,iwe kali zaidi,” alisema.
Akiongeza, alisema pia umri wa dereva wanaoendesha magari ya abiri, nao uangaliwe upya na ikiwezekana, vijana ambao maisha yao yametawaliwa na mbwe mbwe na mihemko iliyopitiliza kama madereva wa kampuni ya mabasi ya City Boy,wasipewe nafasi ya kuendesha magari ya abiria.
Alhaj Mlau aliyasema hayo kwenye swala ya kusherekea Eidd Elfitri iliyofanyika jana kwenye uwanja wa michezo wa Namfua mjini hapa.
Alhaj Mlau alitumia fursa hiyo kuwapa pole jamaa waliofiwa na ndugu zao kwenye ajali ya kugongana uso kwa uso mabasi ya kampuni moja ya City Boy na amemwomba Mungu awajalie nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Kwa upande wake Sheikh wa mkoa wa Singida,Sheikh Salum Mahami,amewakumbusha waumini na jamii yote ya mkoa wa Singida, kuendelea kuiombea nchi ibaki katika amanai na utulivu ,ili waumini wa madhehebu ya dini waendelee kuabudu kwa uhuru mpana na kujiletea maendeleo yao ya kimwili.
Alisema amani na utulivu vikitoweka, kwanza nchi haitakalika, ustawi wa madhehebu ya dini utakuwa shakani na mbaya zaidi, maendeleo ya kijamii hayatakuwepo.
“Maombi haya ya kuiombea nchi yetu, yaendelee sambasamba na kumwombea rais wetu Dk.Magufuli na watendaji wengine wa ngazi mbalimbali ili Mungu awape nguvu na afya, kwa ajili ya kuwatumikia vema wananchi,” alisema.
Na Nathaniel Limu, Singida