Siku chache zilizopita Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla aliweka video katika ukurasa wake wa Twitter kuwa ikimuonyesha akizungumzia taasisi ambazo zimekuwa zikihamasisha watu kushiriki mapenzi ya jinsia moja na kuwa serikali itazichukulia hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuzifuta.
Baada ya taarifa hiyo, Mo Blog ilipata nafasi ya kuzungumza na Dk. Kigwangalla kuhusu hatua ambazo serikali kupitia wizara ya afya inazifanya ili kuzichukulia hatua taasisi zote zinazosaidia watu wanaoshirikia mapenzi ya jinsia moja.
Dk. Kigwangalla alisema wameanza taratibu za kuzichukua hatua taasisi hizo kwa kukutanisha wataalam kutoka wizara mbalimbali ili kufanya kazi ya kuchambua kazi zinazofanywa na kila taasisi ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo ya adhabu ambazo zitachukuliwa kwa taasisi hizo.
“Tumeanza kuchukua hatua na wataalam wa wizara yetu wameungana na wataalam kutoka wizara nyingine ambazo ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jeshi la Polisi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Ofisi ya Waziri Mkuu na watakuwa katika kamati moja wakijadili kuhusu jambo hilo,
“Kamati hii inakazi ya kupitia sera na sheria na baada ya hapo watatoa mapendekezo ya hatua ambazo zitachukuliwa lakini bado hatujayaweka wazi na tutajumuisha na lile ambalo nilisema Mwanza (video aliyoweka Twitter),” alisema Dk. Kigwangalla.
Naibu waziri huyo wa wizara ya afya alisema baada ya mapendekezo ya adhabu, kamati itapitia miradi yote ambayo imeombwa kufanyika kupitia wizara ya afya ili kuifahamu miradi inayojishughulisha kuwasaidia mashoga na kuhamasisha watu kushiriki mapenzi ya jinsia moja.
“Kuna taasisi zikituletea maombi zinakuwa zinaomba vitu vingine wa wanavyofanya ni vitu vingine, kamati itapitia tena miradi inayoombwa kwetu wizara ya afya na taasisi zote ambazo zitakutwa zinahamasiha mapenzi ya jinsia moja zitapewa adhabu ambazo zimetolewa mapendekezo,
“Sijui ni lini watamaliza kazi ya kuzichambua taasisi hizo maana kazi hiyo ni kubwa sababu watapitia mradi mmoja mmoja baada ya hapo taasisi zitakazokuwa zinafanya harakati za kufanyika kwa vitendo hivyo zitachukuliwa hatua na katika hilo tutakuwa serious nchi yetu ina sheria yake na maadili yake,, tutatekeleza hilo,” alisema Dk. Kigwangalla.