DEREVA wa basi la City Boys T.247 BCD Jeremia Martini Sempungwe (33) mkazi wa Kinondoni jijini Dar-es-salaam, jana amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida, kwa tuhuma ya makosa 30 ya kusababisha vifo vya abiria 30 bila kukusudia.
Awali Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, alimwarifu mshitakiwa kuwa atasomewa makosa yake yote na ayasikilize kwa makini. Lakini hatajibu chochote kwa madai kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilza kesi za mauaji.
Baada ya hapo, Mwendasha mashitaka wakili wa serikali mkuu mfawidhi mkoa wa Singida, Zakaria Ndaskoi, alisema kuwa mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la kwenda kinyume na kifungu 195 na 198 cha kanuni ya adhabu sura 16 toleo la kwanza kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Akifafanua, alisema siku ya tukio basi lililokuwa likiendeshwa na mshitakiwa Jeremia likitokea Kahama likielekea jijini Dra-es-salaam, lilipofika eneo la tukio liligongana uso na basi jingine la kampuni hiyo hiyo ya City Boys.
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys, Jeremia Martin Sempungwe
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys, Jeremia Martin Sempungwe (33) mwenye begi mkononi, akisindikizwa mahakamani na askari polisi, kujibu tuhuma ya mauaji ya bila kukusudia.
 “Mheshimiwa hakimu baada ya mabasi hayo kugongana,yalisabaisha abiria 30 kupoteza maisha na kujeruhi wengine 54 vibaya. Kutokana na mazingira yaliyosabaisha vifo hivyo na majeruhi, kumepelekea mshitakiwa ashitakiwe kwa kosa la kuuawa bila ya kukusudia”,alisema wakili huyo mfawidhi wa serikali.
Zakaria aliiambia mahakama hiyo iliyofurika umati wa wasikilizaji, kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilkia na pia mshitakiwa dereva mwingine wa basi T.531 DCE Boniface Mwakalukwa, bado anaendelea kusakwa, ili akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Baada ya kusema hayo,wakili wa kujitegemea mjini Singida, Francis Kitope, alisimama na kuiomba mahakama hiyo impe mteja wake dhamana, kwa madai kuwa kesi hiyo inadhaminika.
Kutokana na ombi hilo,wakili wa serikali Zakaria alisimama na kupinga mshitakiwa asipewe dhamana akidai kuwa wakati huu  si salama kwa mshitakiwa kuwa huru kwa vile tukio bado bichi na ndugu za abiria waliofariki na wale waliojeruhiwa,bado wana uchungu mkubwa.
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys,Jeremia Martin Sempungwe (33) (kulia), akiwa kwenye korido la Mahakama ya Hakimu mkazi mjini Singida, akielekea kwenye chumba cha mahakama kusomewa makosa yanayomkabili ya kuuawa abiria 30 bila kukusudia. Hata hivyo,mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa vile mahakama hiyo, haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
 “Si hivyo tu,washitakiwa wengine wametoroka bado hawajakamatwa wanaendelea kusakwa.Mshitakiwa akipewa dhamana, ataathiri shauri letu”,alisema Zakaria ambaye alikuwa akisaidiwa na Petrida Muta.
Baada ya mabishano hayo,hakimu Minde aliagiza upande wa jamhuri ukaandike pigamizi kwa maandishi, na kisha kuliwasilisha mahakamani ili mahakama iweze kutoa maamuzi.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Julai 21 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, amemtaka dereva Boniface Mwakalukwa aliyefanikiwa kutoroka, ajisalimishe haraka,vinginevyo akikamatwa na polisi atapata adhabu kali zaidi.
Jeremia Martin Sempungwe
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys, Jeremia Martin Sempungwe (33) (mwenye jaketi) akiwa kwenye chumba cha mahakama tayari kusomewa makosa yake 30 ya kuuawa abiria 30 bila ya kukusudia.
Katika tukio jingine,Sedoyeka alisema watu wanne wamefariki dunia baada ya lori aina ya scania T.716 MMM lililokuwa likivuta tela T.391 DCY linalomilikiwa na kampuni ya Hascam Investment  and General Supplies LTD,ya jijini Dar-es-salaam, kutumbukia  darajani katika mlima wa Sekenke wilaya ya Iramba.
Aliwataja watu hao waliofariki  julai saba mwaka huu saa tatu usiku,kuwa ni Thabias Alli (dereva wa lori hilo),wafanyabiashara wa Igunga Christopher Kilindiro (30)na Rajabu Shaban (25) na mwanaume mmoja ambaye hajatambulika.
Aidha,alitaja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Lausius Charles Haule (15) mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Igunga na Marwa Charles (37) mfanyabiashara wa Igunga,wote wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Iramba.
Sedoyeka alisema chanzo cha ajali hiyo ni kufeli kwa breki za lori hilo.
Imeandikwa na Nathaniel Limu, Singida
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys,Jeremia Martin Sempungwe (33) akiwa na wakili wake wa kujitegemea Francis Kitope
Dereva wa basi la kampuni ya City Boys, Jeremia Martin Sempungwe (33) akiwa na wakili wake wa kujitegemea Francis Kitope wakiweka mambo sawa kabla mshitakiwa kupandishwa kizimbani.
Mwendesha mashitaka wakili wa serikali mkuu mfawidhi mkoa wa Singida,Zakaria Ndaskoi
Mwendesha mashitaka wakili wa Serikali Mkuu Mfawidhi mkoa wa Singida, Zakaria Ndaskoi,akitoa ufafanuazi kwa waandishi wa habari juu ya amri ya mahakama ya kutaka wakaandike zuio la kutaka mshitakiwa asipewe dhamana.