Serikali
ya Tanzania inadhamini mchango mkubwa unaotolewa na Serikali ya Japani
kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA) ambalo
limekuwa likishirikiana na Serikali katika kazi mbalimbali za maendeleo
hapa nchini.
Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi. Susan Mlawi
alisema hayo mapema leo katika ukumbi wa mikutano wa Utumishi wakati wa
hafla fupi ya kuwakaribisha watalaam wa kujitolea kutoka Japani.
“Tangu mwaka 1967 hadi sasa zaidi
ya vijana wa Japani 1,500 wameshafika nchini na kufanya kazi za
kujitolea katika maeneo mbalimbali hata katika mazingira magumu” Bi.
Mlawi alisema na kuongeza kuwa kunufaika huko kwa Tanzania kunatokana
na ushirikano baina ya Serikali ya Japani na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Alisema Tanzania itaendelea
kudumisha ushirikiano huo na Japani ili kuendelea kunufaika hasa
katika suala zima la kujengewa uwezo katika sekta ya elimu na maendeleo
ya jamii , sekta ambazo pia zimepewa kipaumbele katika Awamu ya Pili
ya Mpango wa Serikali wa miaka Mitano (5) wa Maendeleo inayoanza mwaka
2016/17 na kumalizika mwaka 2021 /22.
Kwa upande wake, mwakilishi mkuu
wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo Japani (JICA) nchini Tanzania
Bw. Toshio Nagase alisema wataalam hao ambao wako sita (6)
watafanyakazi ya kujitolea katika sekta ya elimu kwa miaka miwili na
kwa kipindi hicho wanaamini Watanzania watakuwa wamenufaika na ujuzi
toka kwa vijana hao.
Alisema watajitolea kufundisha
masomo ya Sayansi, Hisabati, Masuala ya Maendeleo ya Jamii na Michezo
katika shule za Sekondari , Shule za Msingi na Ofisi za Maendeleo ya
Jamii katika Mikoa ya Morogoro, Pwani , Mtwara , Dodoma na Dar es
salaam.
0 maoni:
Chapisha Maoni