Aliyekuwa Rais wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA, Joao Havelange ambaye amefariki jana kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa mapafu akiwa Rio De Janeiro huko nchini Brazil alifanya mengi katika uongozi wake na hata kipindi akiwa hayupo madarakani na jambo kubwa zaidi ni kuwezesha Olimpiki ya Rio 2016 kufanyika nchini kwake.
Havelange aliyemuachia kijiti Sepp Blatter alikuwa Rais wa saba kuongoza Shirikisho hilo kwa muda wa miaka 24 tangu Mei 8 1974 hadi Juni 8 1998 na amefariki akiwa na umri wa miaka 100 tangu alipozaliwa mwaka 1916 May 8 nchini Brazil
Atakumbukwa na mambo mengi aliyoyafanya katika kukuza na kusaidia mpira wa miguu kwa muda wake wote aliokuwa madarakani kwa kuhakikisha kanuni na sheria zote zinafuatwa vizuri kuanzia katika uongozi na hata mambo mbalimbali yanayohusu soka kila kona ya dunia.
Akiwa na elimu ya Sheria, Jina lake lilizidi kuwa kubwa pale alipoongeza washiriki katika kombe la dunia kutoka timu 16 hadi kufikia timu 32 ambapo mashindano ya 6 yalifanyika chini ya Utawala wake.
Havelange aliiwakilisha Brazil katika mashindano ya Olimpiki ya kuogelea mwaka 1936, mwaka ambao aliidhinishwa kuwa mwanasheria kabla ya kuchaguliwa na IOC, Lakini pia alikuwa mmoja kati ya wanakamati wa Olimpiki kuanzia mwaka 1963 hadi 2011 alipojiuzulu kutokana na matatizo ya kiafya.
Alijiuzulu pia nafasi ya Urais wa FIFA April mwaka 2013 kufuatia uchunguzi uliokuwa umefanywa na kutoa ripoti ya madai ya kupokea rushwa na mwaka uliofuatia alilazwa hospitalini kufuatia kukumbwa na ugonjwa wa mapafu.
Joao Havelange ambaye jina lake ni Jean-Marie Faustin Godefroid De Havelange alikuwa alikuwa na ndoto ya siku nyingi kuhakikisha Olimpiki itafanyika kwa nguvu zake nchini Brazil na jambo hilo alilifanikisha ingawa alikuwa amekwishaanza kuumwa.
Na Derick Highiness