Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai kwa jamii kupiga vita mila na tamaduni potofu zinazosababisha kuwepo kwa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike wenye umri kati ya miaka 13 hadi 18.
Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai hiyo wakati alipokuwa akizindua maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani iliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine ameiomba jamii na Mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali kushirikiana kwa pamoja kutokomeza mila hizo.
Amesema kuwa kuwa mfumo dume ndio changamoto kubwa inayowakwaza watoto wa kike kuanzia ngazi ya kaya ambapo kazi za ndani kama za kuosha vyombo, kufagia na kuhudumia nyumba kwa ujumla hufanywa na mtoto wa kike, hali hiyo humpotezea muda mtoto wa kike hatimae kupunguza ushiriki wake katika elimu na mambo mengine ya maendeleo.
Natalia Kanem
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Dr. Natalia Kanem akizungumza kwenye maadhimisho ya hayo.
” Takwimu zilizotokana na utafiti uliofanywa mwaka 2014 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ( NBS) juu ya Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi zimeonyesha kuwa asilimia 43.8 ya watoto wa kike hushiriki katika shughuli za nyumbani zisizo za kiuchumi na kiwango cha wasichana walioajiriwa ni asilimia 47.5 wakati wavulana ni asilimia 52.5 hivyo, tuna kila sababu ya kumkomboa mtoto wa kike”, Amesema Mhe. Ummy.
Amesisitiza kuwa silaha kubwa ya kumkomboa mtoto wa kike ni kumpa elimu bora na ya kutosha pia kupinga mila na tamaduni potofu juu ya watoto hao kwakua ndizo zinazoleta changamoto nyingi zikiwemo za ndoa na mimba za utotoni pamoja na fursa ndogo za kupata elimu na ajira.
Aidha,waziri huyo ametoa wito kwa Watendaji wa Serikali ngazi ya Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya kumlinda mtoto wa kike na kuwekeza katika maendeleo yake pia waendelee kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Elimu inayotoa katazo la kuoa au kuolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 19.
Amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa jitihada zao za kuwajengea wasichana uwezo wa kujitambua na kufahamu masuala mbalimbali ya kijamii yanayoendelea pia ametoa wito kwa wadau kuangalia namna ya kuwafikia wasichana wengi waliopo maeneo ya vijijini.
Imeandaliwa na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mh. Ummy Mwalimu