Siku moja baada ya serikali kutoa taarifa ya kuvifungia baadhi ya vituo ambavyo vinatoa tiba asili kwa sababu kuwa vimekuwa vikijitangaza kutoa tiba ya kisasa, Baraza la Waganga wa Tiba, Ushauri na Utafiri wa Dawa Asili Tanzania (BAWATA) limejitokeza mbele ya waandishi wa habari na kupinga agizo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa BAWATA, Shariff Daudi Bin Wiketye alisema kuwa serikali imefanya maamuzi hayo bila hata kuwasikiliza waganga ambao wanatoa tiba katika vituo hivyo ili kupatiwa ufafanuzi zaidi kuhusu kazi zao.
Alisema kuwa BAWATA inaamini kuwa kufungiwa kwa vituo hivyo kunasababishwa na ubinafsi uliopo kwa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lakini pia kuongozwa na watu ambao wamesoma elimu ya kisasa hivyo hawaamini kama tiba asili inaweza kufanya kazi.
“Tunasikitishwa sana na utendaji kazi wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ambalo lipo chini ya serikali na badala ya kufanya kazi kuinua tiba asili ndiyo limekuwa mbele kukandamiza juhudi zinazofanywa na waganga wa tiba asili,
“Bado tunajiuliza sababu kubwa ni nini maana wamefanya maamuzi bila hata kuwaita waganga ili wawahoji lakini tunahisi kuwa maamuzi hayo yanafanywa sababu baraza linaongozwa na watu wanaoamini kisasa (hospitali) au wengine wana biashara ya tiba asili hivyo wanafungia wengine ili wao biashara yao ifanyike vizuri,” alisema Daudi.
Aidha alisema kuwa haoni sababu ya wao kuzuiliwa kutumia jina la udaktari na kuvaa makoti ya rangi nyeupe na hivyo kuiomba serikali kuwaruhusu kufanya kazi zao kama awali walivyokuwa chini ya wizara ya elimu kwani kwa sasa wanafanya kazi zao chini ya wizara ya afya ambayo wanaamini haiwatendei haki.
“Wakati tupo wizara ya elimu tulikuwa tunafanya kazi vizuri lakini sasa hivi tunabanwa, niiombe serikali kupitia rais wetu Dk. Magufuli ituruhusu kutumia jina daktari na kuvaa makoti ya rangi nyeupe, sasa hivi wanasema hatuna vigezo lakini awali tulitumia jina na makoti hayo tunaomba waturuhusu tena kuendelea kutumia kama awali,” alisema Daudi.