Kikosi Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara timu ya Yanga kimeondoka hii leo kuelekea nchini Angola kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa marudiano dhidi ya wenyeji wao timu ya Sagrada Esperanca.
Kikosi hicho ambacho kinatarajiwa kupambana na Esperanca siku ya Jumatano katika mchezo huo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kimewaacha wachezaji wake wanne.
Wachezaji hao ambapo wameachwa katika msafara wa kikosi hicho ni kipa Benedicto Tinocco ambaye hayumo kwenye programu za mchezo sawa na viungo Said Juma na Issoufou Boubacar wakati Malimi Busungu ni majeruhi.
Katika mchezo huo, Yanga itahitaji hata sare kusonga mbele, baada ya awali kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao yaliyowekwa nyavuni na Simon Msuva na Matheo Anthony.
Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
Kikosi cha Yanga kilichoondoka hii leo ni Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
Mabeki; Juma Abdul, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Viungo; Thabani Kamusoko, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony, Amissi Tambwe na Paul Nonga.
Huku benchi la ufundi likiwa na Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm (Uholanzi)
Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi
Kocha wa makipa; Juma Pondamali
Daktari; Edward Bavu
Mchua Misuli; Jacob Onyango
Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo
Meneja; Hafidh Saleh
0 maoni:
Chapisha Maoni