|
SERIKALI
imeondoa ushuru wa mazao kwenye mageti na sasa yatatozwa ushuru
yanapofika sokoni tu, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba
amelieleza Bunge.
Kwa sasa
mazao yamekuwa yakitozwa ushuru yanapofika mipaka ya kata kwenye mageti
maalumu na hata yanaporudishwa mashambani, hali ambayo imekuwa
ikilalamikiwa sana na wakulima nchini.
Mwigulu
alieleza hayo wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni
mjini hapa jana. Katika mwaka ujao wa fedha, wizara hiyo imeomba
kuidhinishiwa Sh 275,063,518,000.
Vilevile
aliwatangazia neema wakulima kwa kuwaambia sasa pembejeo za kilimo
zitapatikana kwa wingi akifafanua, “zitapatikana kama Coca- Cola
dukani.” Alisema wizara inapitia upya mfumo wa sasa wa vocha za pembejeo
kwa lengo la kupata mfumo utakaowezesha upatikanaji wa mbolea kwa
wakulima wote wanaohitaji kupitia maduka ya pembejeo kwa bei nafuu.
“Mbolea
inategemewa kupatiwa ruzuku kutokea kwenye chanzo chake kabla
haijaingizwa nchini. Wizara tunapendekeza ipatiwe fedha zitokanazo na
ushuru wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazowasilishwa Hazina ili
zitumike kuboresha miundombinu na upatikanaji wa ruzuku katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema.
Akizungumzia
ugonjwa wa ebola, Mwigulu alisema mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara ya
Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na
Chakula (FAO), watachunguza uwepo wa virusi vya ugonjwa huo viitwavyo
Filoviridae katika mbuzi na nguruwe kwenye maeneo yanayopakana na mbuga
za wanyama.
Alisema
serikali itajenga kituo maalumu mkoani Dar es Salaam cha kudhibiti ubora
na usalama wa maziwa na kurasimisha wachuuzi wa maziwa kufanya biashara
endelevu. Alisema katika mwaka 2016/2017, wizara hiyo itaandaa
utaratibu wa kuanzisha upya Shirika la Uvuvi Tanzania kwa lengo la kuwa
na meli za kitaifa, zitakazokuwa zinavua bahari kuu.
Kwa
upande wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa kambi hiyo kwa Wizara ya
Kilimo, Magdalena Sakaya alisema hadi Machi 31, mwaka huu, wizara hiyo
ilikuwa haijapokea hata shilingi moja kati ya Sh bilioni 19.4 kwa ajili
ya utekelezaji miradi ya maendeleo.
Sakaya
alisema kambi ya upinzani inaitaka serikali kuja na mpango wa dharura wa
mwaka 2016/2017, kuhakikisha kuwa kunakuwa na usafi na vifaa bora vya
kusafirisha nyama katika machinjio nchini.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk
Mary Nagu akisoma maoni ya kamati yake, aliitaka serikali kuandaa
utaratibu maalumu utakaowezesha ushirikishwaji wa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kufanya doria ili kudhibiti vitendo vya
uvuvi haramu, hasa katika kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu hasa katika
kudhibiti uvuvi wa kutumia mabomu.
0 maoni:
Chapisha Maoni