………………………………………
Baada ya kuanza rasmi kwa mabasi
ya mwendo wa haraka Jijini Dar es Salaam wananchi wameupokea kwa maoni
tofauti huku wengi wao wakisifia hatua hiyo ya serikali katika
kurahisisha hali ya usafiri katika jiji hilo.
Wakitoa maoni yao katika maeneo
mbalimbali ya jiji ,Bw.Kulwa Khamis Mfanyabiashara, mkazi wa Mbezi
mwisho amesema kuwa huduma hii ya usafiri ni nzuri kwa kuwa haina foleni
na inaokoa muda wa kusafiri.
“nimefurahishwa na huduma hii kwa
kuwa haina foleni na inasaidia kufika kwa wakati maeneo yetu ya kazi na
hata kurudi nyumbani mapema,jambo ambalo linapunguza muda mwingi
uliokuwa ukipotea katika foleni” alisema Bw.Khamis.
Naye Bi.Emmy Jonas mkazi wa
Kibamba amesema kuwa huduma hiyo ni nzuri lakini amedai kuwa nauli ni
kubwa na kuomba uongozi wa Dar es Salaam Rapid Transport (DART) na
taasisi husika kufikiria upya nauli ili wananchi wa hali ya chini
waweze kumudu.
Aidha Bi. Jonas ameiomba serikali
kumalizia miundombinu ya barabara ya mabasi yaendayo kwa haraka (BRT)
ili yaweze kufika mpaka Kibaha, badala ya Kimara mwisho ili kuepukana na
usumbufu wa kupanda magari.
Kwa upande wake Mtaalam wa
Mawasiliano wa BRT, Bw. Abraham Nyatori ameiomba jamii ibadilike
kuhusu utunzaji wa miundombinu,“hakuna kitu kinaitwa mali ya
umma”,amesisitiza Nyatori.
Mtaalam huyo alikuwa na maana
kwamba kila mwananchi anatakiwa kulinda na kuitunza miundombinu ili
itumike kwa muda mrefu na kuiona kama mali yake na siyo ya umma.
Serikali imekuwa ikijenga barabara
katika maeneo mbalimbali jijini na baadhi ya barabara hizo kuharibika
baada ya muda mfupi na hivyo kuigharimu serikali mamilioni ya fedha
kwa ajili ya matengenezo badala ya kujenga barabara zingine .
0 maoni:
Chapisha Maoni