……………………………………………….
Halmashauri ya Wilaya ya
Morogoro imeviwezesha Vikundi 39 vya Wanawake pamoja na Vijana vyenye
wanachama 295 kupatiwa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 23.8 kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake.
Taarifa hiyo imetolewa
leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) wakati
akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini, Mhe. Tebweta Omary
lililotaka kujua mpango wa Serikali wa kuzibana na kuziamuru
Hallmashauri zote ikiwemo ya Morogoro Vijijini kutenga asilimia 5 ya
fedha za mapato ya ndani kwa Vijana na asilimia 5 kwa ajili ya akina
mama.
Mhe. Jafo amesema
kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2015/16, Serikali imetenga shilingi
milioni 175 kwa ajili ya wanawake na vijana kutokana na mapato ya ndani.
Amefafanua kuwa,
mkakati wa sasa wa Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili
kujenga uwezo wa kutenga fedha zaidi ambapo katika bajeti ya mwaka wa
fedha wa 2016/17 sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila
Halmashauri lilikuwa ni kuonyesha asilimia 10 zilizotengwa kwa ajili ya
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake kutokana na mapato ya ndani.
“Halmashauri zote
zimeagizwa kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa kwenye vikundi husika
ikijumuisha walemavu na kusimamia marejesho yake ili vikundi vingine
viweze kunufaika.
Kwa upande mwingine,
Mhe. Jafo amejibu swali la Mbunge wa Geita Mjini, Mhe. Kanyasu
Costantine John ambaye alitaka kujua kwanini Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Nyankimbo imabaki kuwa shule ya Kutwa wakati mazingira yake
yanafaa kuwa sekondari ya Bweni ambapo alijibu kuwa shule hiyo
ilijengwa chini ya Mradi wa Geita Giold Mining na kupata usajili wa Na.
S.1942 mwaka 2006 ikiwa ni shule ya kutwa kwa kidato cha Kwanza hadi cha
Nne.
Aidha, amesema kuwa
mwaka 2012 shule hiyo iliongezewa kidato cha Tano na Sita hali
iliyoifanya shule hiyo kuwa imesajiliwa ya kutwa kwa kidato cha kwanza
hadi cha nne na Bweni kwa kidato cha Tano na Sita.
“Taratibu zilizotumika
ili kuisajili shule kuwa ya bweni ni Halmashauri yenyewe kuwasilisha
maombi Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ili kupata
kibali”, alisema Mhe. Jafo.
Aliongeza kuwa, kabla
ya kupata usajili, Kamishna wa Elimu atatuma Timu ya Wataalam katika
shule husika kwa ajili ya kuhakiki uwepo wa miundombinu inayohitajika
ilio shule iweze kusajiliwa kuwa ya bweni.
0 maoni:
Chapisha Maoni