Wabunge wanawake kutoka UKAWA, wametoka bungeni kufuatia Mbunge wa wa Ulanga, Mhe. Goodluck Mlinga kusema kuwa wabunge wa viti maalum kutoka UKAWA wanapewa nafasi hizo kwa kuwa na mahusiano na viongozi wa juu wa vyama vyao.
Baada ya kutamka maneno hayo, mmoja wa wabunge wa viti maalum aliomba mwongozo kutoka kwa Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson na alipoona kuwa hapewi nafasi wabunge wanawake wa upinzani kwa pamoja walisimama na kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka nje ya bunge, Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa BAWACHA, Halima Mdee amesema wanaumia wao kama wabunge wanawake kufanyiwa vitendo hivyo na spika akiwa ni mwanamke bila kuchukua hatua yoyote.
Amesema sababu ya kuomba mwongozo ilikuwa ni kumtaka, Mhe. Mlinga afute kauli aliyoisema awali lakini hakuna hatua iliyochukuliwa na kwasababu spika ameshindwa kuchukua hatua kwa pamoja wabunge wa UKAWA wanaandika barua ya kujitoa Chama ca Wabunge Wanawake (TWPG).
“Tunajua nchi hii bado ina mfumo dume lakini usifike hii na kila tukikutana katika vikao vya Chama cha Wabunge Wanawake tunazungumza lakini hata leo spika ni mwanamke lakini hajafanya kitu,
“Mhe.  Mlinga anasema wabunge wa viti maalum kutoka UKAWA wanaingia bungeni mpaka wawe na mahusiano na viongozi na sisi tuna taratibu zetu kama chama ili kumpitisha mbunge lakini kama ni hivyo hata wao wabunge wao wanalala na viongozi wao ndiyo wanawapa nafasi,”  alisema Mhe. Mdee na kuongeza.
“Kwa pamoja wabunge wanawake wa upinzani tumekubaliana kuandika barua kujitoa TWPG na tuwaachie chama chao kiwe Chama cha Wabunge wa CCM”