Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandishi Mathew Mtigumwe, amtumbua jipu (amsimamisha kazi) kwa muda usiojulikana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Simion Mumbe kwa tuhuma ya kutoa taarifa ya udanganyifu kuwa watumishi hewa 19 wa halmashauri hiyo hawajaisababishia hasara serikali.
Akizungumza jana kwenye ufunguzi wa kikao cha maendeleo cha mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Mtigumwe, alimwagiza Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Angela Mageni  Lutambi, kumwandikia Mumbee mara moja barua ya kumsimamisha kazi kupisha uchuguzi zaidi.
Akifafanua, alisema kuwa Mumbee katika taarifa yake ya watumishi hewa, alionyesha kuwa na watumishi hewa 19, lakini akabainisha kuwa watumishi hao hawajaisababishia hasara yoyote serikali.
“Nilipotuma tume kufuatilia suala la watumishi hewa katika halmashauri ya wilaya ya Singida, ilibaini kuwa watumishi hao hewa, wameisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi 125 milioni,” alisema  na kuongeza.
“Kwa jumla taarifa ya Mumbee ililenga kudanganya jambo ambalo ni baya sana na si kubaliani nalo kabisa. Halmashauri ya wilaya ya Singida hivi sasa mhasibu wake amefikishwa mahakamani akituhumiwa kujiingizia  kwenye akaunti yake ya benki mishahara 11 ya watumishi hewa, sasa itakuwaje mkurugenzi aseme hakuna hasara iliyosababishwa na watumishi hewa”.
Mhandisi Mtigumwe kwa masikitiko, alisema kuwa hana nafasi ya kufanya kazi na watumishi aina ya Mumbee ambao wanatoa taarifa za udanganyifu huku serikali ikiingia hasara kubwa.
“Wakuu wa wilaya nawaombeni sana mnisaidie kupambana na watumishi wa umma wenye tabia kama ya Mumbee ya kutoa taarifa za udanganyifu. Kwa njia hiyo mtakuwa pia mnamsaidia rais wetu katika vita vya kupambana na watumishi hewa,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa, alipomaliza kufungua kikao hicho, Afisa Tawala Mkoa alitoa nafasi kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Singida, kutoa taarifa yake ya madawati katika shule zake.
Mumbee ambaye alionyesha dhahiri kupigwa mbumbuwazi na agizo la kusimamishwa kazi, alisimama ili aweze kuisoma taarifa hiyo ambayo alikuwa nayo.
Bila shaka Mumbee aliamini kuwa atasimama kufanya kazi pale atakapopewa barua ya kusimamishwa hivyo alisimama tayari kuanza kuisoma taarifa hiyo.
Lakini ghafla mkuu wa mkoa, aliingilia kati na kumwambia Mumbee kwamba kwa wakati huo hakuwa mtumishi wa umma kwa vile amemsimamisha kazi. Alimwagiza kazi ya kusoma taarifa hiyo amkabidhi mtumishi mwingne na yeye aondoke kwenye mkutano huo.
Mumbee kwa unyonge aliacha karatasi za taarifa hiyo juu ya meza na kuondoka kwa miguu hatua zaidi ya mia mbili kurudi ofisini kwake kuchukua vilivyo vyake. Wakati wa kwenda kwenye kikao hicho, Mumbee alikwenda na gari lake la kazi.
Na Nathaniel Limu, Singida
IMG_5054Mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew John Mtigumwe,a kitangza rasmi uamuzi wa kumtubua jipu (kumsimamisha kazi), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Simion Mumbee, kwa tuhuma ya kutoa taarifa ya udanganyifu kuhusu watumishi hewa.
IMG_5060Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Simion Mumbee (mwenye koti jeusi) akisikiliza kwa makini agizo lililokuwa linatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe la kumsimamisha kazi.
IMG_5061
IMG_5062Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Simion Mumbee akijiandaa kusoma taarifa yake ya madawati hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe alimzuia kwa madai kuwa tayari alikuwa si mtumishi tena wa umma.
IMG_5063Picha ya juu na chini ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Simion Mumbee akirejea kwa miguu ofisini kwake baada ya kusimamishwa kazi na mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe. (Picha na Nathaniel Limu)
IMG_5064