……………………………
Serikali imewaunga mkono
Wachimbaji Wadogo wa Madini wa Busiri kwa kuwatafutia maeneo ya
uchimbaji wa madini, ambapo Wizara ya Nishati na Madini imetenga eneo
lenye ukubwa wa hekta 11,031 lililokuwa chini ya Leseni za Utafutaji
namba PL 3220/2005 ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Bw. Daudi Mbaga pamoja
na PL 5853/2009 iliyokuwa ikimilikiwa na na Meru Minerals Resources
Limited ambazo zilizoisha muda wake.
Hayo yamesemwa leo Bungeni mjini
Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Nishati na Madini, Mhe. Medard
Kalemani wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi
kuhusu mikakati ya Serikali ya kuwaunga mkono Wachimbaji wadogo wadogo
wa Busiri.
Mhe. Kalemani ameeleza kuwa,
hadi mwishoni mwa mwezi Machi, 2016, Wizara yake imegawa kwa wananchi wa
Busiri leseni 81 za Uchimbaji Mdogo wa Madini (PMLs) katika eneo hilo,
sawa na takribani hekta 810 kati ya hekta 11,031 za eneo lililoachwa kwa
ajili ya Wachimbaji Wadogo.
“Wizara imegawa leseni nyingine
30 za uchimbaji mdogo (PMLs) katika eneo lililopo katika kijiji cha
Kuntakama takribani kilomita moja eneo la uchimbaji mdogo wa madini la
Busiri”, alisema, Mhe. Kalemani.
Ameongeza kuwa, mkakati mwingine
wa Serikali ni kuendelea kulitumia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)
kutoa huduma ya ugani kwa wachimbaji madini wadogo wa kijiji cha Busiri
na wengine wote nchini ikiwemo kutoa ruzuku kupitia Mfuko wa Wachimbaji
Wadogo.
“STAMICO pia itaendelea kuwapa
elimu wachimbaji wadogo na kuwahamasisha kuunda Vikundi vya Uchimbaji
ili waweze kusaidiwa kwa pamoja”, alisema Mhe. Kalemani.
Aidha, Serikali imekuwa
ikiwatembelea wachimbaji madini wa eneo tajwa mara kwa mara kwa kutumia
Maafisa na Wataalamu wa Ofisi ya Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi na
Ofisi ya Afisa Madini Mkazi-Bukoba.
Amefafanua kuwa, tarehe 11
Machi, 2016 Afisa Madini Mkazi wa Bukoba alifika na kufanya mkutano na
kikundi cha Busiri Mining Co-operative Society Limited chenye Leseni Na.
PML 001712WLZ.
“Ili kutekeleza ombi la sasa la
Mheshimiwa Mbunge, Wizara yangu itamtuma Afisa Madini wa Kanda ili
awatembelee tena na kuwaelimisha juu ya fursa zilizopo za kuendeleza
wachimbaji wadogo ili uchimbaji uwe wenye tija na kutoa ajira na kuondoa
umaskini kupitia uchimbaji wa madini”, aliongeza, Mhe. Kalemani.
0 maoni:
Chapisha Maoni