|
CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM) kimesema hakuna mgogoro wowote katika mchakato wa
kukabidhi kijiti cha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho kutoka kwa
Mwenyekiti wa sasa Jakaya Kikwete kwenda kwa Rais John Magufuli.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Msemaji wa CCM
Taifa, Christopher ole Sendeka ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM (NEC) ilieleza taarifa hizo zinazushwa na baadhi ya
vyombo vya habari visivyozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa
habari.
“Baadhi
ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa potofu kuhusu mchakato wa
Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dk Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti cha uongozi
wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo mila na desturi ya CCM.
“Yamekuwapo madai eti Mwenyekiti amekataa au anachelewesha kukabidhi
kijiti.
Habari
hiyo si kweli kabisa na ni kinyume chake, kwani Dk Kikwete amekuwa
akisisitiza kukabidhi madaraka mapema iwezekanavyo. “Kwa ajili hiyo
kwenye kikao cha Mei 3, 2016 alikataa kusiongezwe ajenda nyingine ambazo
zitalazimisha Mkutano Mkuu Maalumu kuchelewa kufanyika kwa sababu ya
kukamilisha maandalizi ya ajenda hizo na alisisitiza ajenda iwe moja
tu,” ilieleza taarifa hiyo ya CCM.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo ya Ole Sendeka, dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu
Maalum Juni, 2016 iko pale pale na kwamba kilichoelezwa kwenye kikao ni
kutaka kukamilisha utaratibu wa kupata fedha za kugharimia mkutano huo.
“Taratibu
zikikamilika tarehe itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa inaendelea na
ikikamilika tarehe itatangazwa,” alisema Msemaji huyo wa CCM Taifa.
Aliwataka wana-CCM wasihamanike wala kubabaishwa na taarifa za
upotoshaji zinazofanywa na watu wenye nia mbaya na chama hicho, akisema
watu hao ni wale ambao wamekuwa wakiiombea mabaya CCM bila ya mafanikio.
“Pia
tunapenda kukanusha madai ati kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwatahadharisha
wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu ukimya wa Edward Lowassa. Hakuna wakati
wowote kauli kama hiyo aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la Ndugu Lowassa
halikutajwa kabisa,” alisema.
Katika
hatua nyingine Ole Sendeka alikanusha madai ya kufanyika mkutano baina
ya Mwenyekiti Kikwete, Rais Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, kuhusu uchaguzi wa Katibu wa
Kamati ya Wabunge wa CCM.
0 maoni:
Chapisha Maoni