………………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) yatoa mkopo wa 890 Milioni kwa wakulima wa zao la mpunga
wanaojishughulisha kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Mkula
wilayani Kilombero ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga.
Hayo yaliwekwa bayana na
Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Bw. Robert Paschal wakati wa
warsha ya wakulima wadogo zaidi ya 340 wa Mkoa wa morogoro iliyofanyika
katika Ukumbi wa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Bw. Paschal alisema lengo la
mkopo huo unaowanufaisha zaidi ya wakulima 350 ni kuongeza tija na
uzalishaji wa mpunga ili Kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama
wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania na kuchagiza na kusaidia
Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara
ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
“Mkopo huu na mengine tunayotoa
imelenga kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo ili kusaidia
kukabiliana na mapungufu hayo na kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika
sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika kilimo nchini,” alisema Bw.
Paschal.
Kwa mujibu wa Bw. Paschal mkopo
huo utasaidia shughuli mbalimbali za utayarishaji wa mashamba, kupima
ubora wa udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye uzalishaji wa
mpunga pamoja na kuwezesha upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo
mbegu bora, mbolea na madawa.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa
Benki imetoa mkopo kwa ajili ya uwekezaji kwenye ujenzi viwanda vya
kusindika mazao, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa mitambo ya usindikaji
wa mpunga ili kuongeza thamani wa zao hilo.
“Tunaamini mkopo huu utachagiza
kuongezeka kwa upatikanaji wa chakula na Pato la Taifa kutokana
kuongezeka kwa tija na uzalishaji hivyo kuwa chachu ya ongezeko la
thamani, ukuaji wa viwanda vya mazao ya kilimo hivyo kuchangia
kuongezeka kwa ajira nchini,” aliongeza.
Akizungumzia mikakati ya TADB kwa
sasa, Bw. Paschal alisema Benki imejipanga kutoa mikopo ya Muda Mfupi,
Mikopo ya Muda wa Kati na Mikopo ya Muda Mrefu kwa kutumia njia
mbalimbali. Mbinu hizo zinajumuisha pamoja na mambo mengine; mikopo ya
moja kwa moja kwa vikundi vya wakulima wadogo wadogo; kutoa mikopo kwa
njia ya marejesho taasisi zinazokopesha; utoaji wa mikopo kwa pamoja na
kushirikiana na taasisi/benki zingine; pamoja na mikopo ya miundombinu
inayolenga kupunguza mapengo ya upatikanaji wa fedha katika minyororo ya
ongezeko la thamani ya kipaumbele.
“Kwa kuanzia, TADB imelenga
uwekezaji katika maeneo nane (8) ya minyororo ya uongezaji wa thamani
ambayo ni: nafaka, kilimo cha mboga mboga, kilimo cha bidhaa za viwanda,
mbegu za mafuta, ufugaji wa ng’ombe, ufugaji kuku, ufugaji wa samaki na
bidhaa za misitu. Benki pia inajitahidi kusimamia fedha kutoka kwa
wafadhili wengine ambazo zimeelekzwa kwenye kuendeleza kilimo,” alisema.
Warsha hiyo ilifunguliwa na Mkuu
wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Lephy Gembe ambaye alitoa rai kwa Wakulima
wote waliopata fursa ya kuhudhuria warsha hiyo kujipanga katika
kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na TADB.
Mhe. Gembe zingatia mada
zilizowasilishwa ili waweze kunufaika na Benki hii na shughuli
zinazotolewa na Taasisi zingine za serikali
“Nawasihi mrudishe mikopo
mtakayopewa kwa wakati ili wakulima wengine waweze kunufaika zaidi na
Benki hii na vile vile kuwezesha Benki kutoa huduma kwenye maeneo
mengine ya Tanzania,” alisema.






0 maoni:
Chapisha Maoni