Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Alli Hapi amemtaka mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuwavua madaraka wakuu wa shule za msingi 68, pamoja na kumuandikia barua Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwavua vyeo wakuu wa shule za sekondari 22.
Hapi alitoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kufanya uhakiki na kubaini kuna wanafunzi hewa zaidi ya 5000 katika shule za msingi na sekondari katika manispaa hiyo.
“Rais Magufuli alitoa agizo akiwa Shinyanga kwa wakuu wa wilaya kufanya uhakiki wa wanafunzi ili kubaini kama wana sifa na vigezo vya kupewa ruzuku ya elimu bure,” amesema.
Amesema baada ya uhakiki kufanyika ilibainikia kuwa wakuu hao wa shule walifanya udanganyifu.
“Wamefanya udanganyifu kwa maslahi yao binafsi kufuatia hilo mkurugenzi wa manispaa atawavua madaraka wakuu wa shule za msingi waliofanya udanganyifu,” amesema.
Ameongeza “Pia mkurugenzi amuandikie barua katibu tawala wa mkoa kuwavua madaraka wakuu wa sekondari vilevile majina ya waalimu hao yapelekwe Tume ya Utumishi ya Walimu ili hatua nyingine za kinidhamu zifuatwe,” amesema.
Amesema wanafunzi waliobainika kutokuwa na sifa za kupata ruzuku hizo ni 3462 katika shule za msingi 68, na 2534 katika shule za sekondari 22 ambao hawajaandikishwa kwenye kitabu cha takwimu.
“Serikali kila mwezi inapoteza Bilioni 18.8 kwa ajili ya kugharamia elimu bure hivyo udanganyifu uliofanywa ni ukosefu wa maadili na uzalendo,” amesema.