Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi wa Kampuni ya Estim Construction anayejenga Daraja la Ruvu Chini linalounganisha barabara ya Bagamoyo-Msata yenye urefu wa Km 64 mkoani Pwani kukamilisha ujenzi wa daraja hilo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Prof. Mbarawa amesema hayo wakati alipokagua ujenzi wa Daraja hilo na kuhimiza kukamilika kwa wakati uliopangwa ili kuhakikisha barabara hiyo inapitika majira yote ya mwaka na kurahisisha huduma ya usafiri kwa wakazi wa mkoa wa Pwani na mikoa jirani.
“Hakikisheni ujenzi wa Daraja hili unakamilika kwa wakati ili lianze kutumiwa na wananchi kwa wakati wote kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao binafsi,” alisema Prof.Mbarawa.
Vile vile Profesa Mbarawa amemhimiza Mkandarasi huyo kuzingatia viwango vya ubora kulingana na thamani ya fedha ili Daraja hilo liweze kudumu kwa muda mrefu.
“Ni vema daraja hili lijengwe kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha ili liweze kuhimili athari za Mvua zinajitokeza eneo hili,” alisisitiza Waziri Mbarawa.
Aidha Waziri Mbarawa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika miradi inayotarajiwa kuanza kutekelezwa maeneo mbalimbali nchini.
Zaidi ya Shilingi Bilioni 129zitatumika katika ujenzi wa Barabara ya Msata-Bagamoyo Km 64, Daraja la Ruvu chini yenye urefu wa Mita 140 pamoja na Barabara ya Maingiliano ya Daraja hilo yenye urefu KM 4.2.