Mkuu wa mkoa wa Singida,mhandisi Mathew Mtigumwe (kulia), akimwapisha mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu
Mkuu wa mkoa wa Singida, mhandisi Mathew Mtigumwe (kulia), akimwapisha Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu. Hafla hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa mjini Singida.Picha na Nathaniel Limu.
 




MKUU mpya wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtafuru, amesema kipaumbele chake cha kwanza katika kuwatumikia wananchi, ni kuhakikisha wananchi wote wanaondokana na dhana potofu kwamba serikali pekee ndiyo yenye jukumu la kuiletea wilaya hiyo maendeleo.
Amesisitiza kwamba dhana hiyo yenye lengo la kudumaza dhana maendeleo ya wilaya hiyo changa,itafika wakati itabaki kuwa ni historia.
Wananchi wote watabadilika na kuwa na fikra sahihi kwamba maendeleo ya kweli ya wilaya ya Ikungi, yataletwa na wao wenyewe.
DC Mtaturu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi  baada ya kuapishwa na Mkuu wa mkoa mhandisi Mathew Mtigumwe kwenda kuongoza wilaya hiyo pekee mkoani Singida, iliyopo mikononi mwa Chama cha Upinzani (CHADEMA).
“Hatutakubali mtu yeyote au kiongozi yeyote atumie elimu yake kudumaza maendeleo ya wilaya ya Ikungi. Popote duniani, wananchi ndio wanaochangia kwa hali na mali maendeleo yao. Dhana hii potofu kwamba serikali pekee ndio yenye jukumu la kuiletea maendeleo ya wilaya ya Ikungi, tutaipiga vita kwa nguvu zetu zote”,alifafanua zaidi.

Aidha, amesisitiza kwamba atahakikisha wananchi wa wilaya hiyo changa ya Ikungi hawatumiki vibaya na wanasiasa au mtu mwingine ye yote mwenye lengo la upoteshaji.
Katika hatua nyingine, Mtaturu alisema atasimamia kikamilifu elimu bora itakayokidhi mahitaji ya karne hii inatolewa, ili wilaya hiyo iendelee kupata vijana wengi wasomi ambao baadaye wataziendeleza familia zao kiuchumi na kijamii.
“Tukiwa na vijana wengi wasomi, wakulima wa wilaya yetu watalima na kufuga kitaalamu na hivyo shughuli hizo zitakuwa na tija zaidi. Kwa ujumla wasomi ndio watakaosaidia wilaya ya Ikungi kupaa kimaendeleo na ikiwezekana ipite wilaya kongwe”,alisema kwa kujiamini.
Hata hivyo,alisema hayo yote pamoja na maendeleo ya sekta zingine muhimu, yatafanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa vile atashirikisha watendaji wote wa ngazi mbalimbali na wapenda maendeleo wa wilaya hiyo.
Wakati huo huo,Mtaturu ametumia fursa hiyo kumshukuru rais Dk. Magufuli kwa kitendo chake cha kumwamini na kumteua kama mkuu wa wilaya ya Ikungi,na kuahidi kwamba hatamwangusha.
Imeandikwa na Nathaniel Limu