Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya Usalama vilivyopewa jukumu la kutengeneza madawati kujipanga zaidi ili kutekeleza kwa wakati majukumu wanayopewa.
Mhe. Rais aliitoa kauli hiyo leo, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango wa ugawaji wa madawati yaliyotolewa na Ofisi ya Bunge kwa Majimbo 155 ikiwa ni awamu ya kwanza ya ugawaji wa madawati hayo.
Mnamo April 11, 2016 Mhe. Rais alipokea hundi ya shilingi Bilioni Sita kutoka Ofisi ya Bunge na kuagiza fedha hizo zielekezwe katika utekelezaji wa utengenezaji wa madawati ambapo Magereza na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) walipewa jukumu la kutengeneza madawati hayo.
Aidha Mhe. Rais amesikitishwa na kasi ambayo JKT na Magereza wametumia katika utengenezaji wa madawati hayo, ambapo kwa miezi mitatu wametengeneza jumla ya madawati elfu Sitini.
“Nina wasiwasi na kasi yenu, ikiwa kwa miezi mitatu mmetengeneza madawati elfu sitini basi kuna uwezekano wa zoezi hili la utengenezaji wa madawati mkamaliza mwaka 2017,” alifafanua Mhe. Rais.
Aliendelea kwa kusema kuwa, suala la madawati ni la haraka alihitaji kusubiri kwa muda mrefu hivyo vyombo hivyo vinatakiwa kutengeneza madawati hayo kwa uharaka kwani nguvu kazi ya kutosha wanayo.
Kwa upande wake, Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson amesema kuwa Ofisi ya Bunge inategemea kugawa madawati 120,000 kwa awamu mbili tofauti ambapo awamu ya kwanza imekamilika na jumla ya madawati 61,385 yatagawiwa kwa majimbo 155 kati ya majimbo 264.
Fedha iliyotolewa na Ofisi ya Bunge ni Fedha iliyotokana na matunda ya mpango wa Serikali wa kubana matumizi ambapo Ofisi ya Bunge imeweza kubana matumizi na kubaki na Shilingi Bilioni Sita kwa mwaka wa fedha 2015/2016.