-Adai aligongwa na gari la mkuu wa mkoa wa Mbeya mwaka 1980
-Ulemavu umemfanya ashindwe kumudu maisha
-Aomba alipwe fidia ajengewe nyumba
Kikao cha kusikiliza kero cha Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla kwenye ukumbi wa Mkapa kilikumbwa na taharuki baada ya kuibuka mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Gibson Mwasembo(60) aliyedai kugongwa na gari la Mkuu wa mkoa wa Mbeya mwaka 1980 na kupata ulemavu.
Mwasembo anadai kuwa aligongwa na gari aina ya Landrover yenye namba za usajili STF 933 ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyemtaja kwa jina la Julius Mbaga na kupata ulemavu wa kudumu.
”Wakati nagongwa na gari nilikuwa na umri wa miaka 24 sasa hivi nina miaka 60 kabla ya hapo nilikuwa ni mzima ninayetembea vizuri na kufanya shughuli zangu kama kawaida nilipata ulemavu baada ya kugongwa na gari,”alifafanua
Alisema amekuwa akifuatilia fidia na haki yake kwa miaka mingi bila mafanikio ambapo awali katika kesi hiyo ya Trafiki mahakama iliamuru mshtakiwa dereva wa gari hilo alipe faini sh.3,000 au kwenda jela miezi 9, dereva alilipa faini na kuachiwa huru.
‘’Fidia ililipwa mahakamani, mimi nikabaki na ulemavu maisha yangu yamekuwa ya kubangaiza, nasafiri kuja Mbeya kufuatilia haki yangu, nalala stendi Kuu ya Mabasi, namuomba Mheshimiwa Makalla anisaidie,’’alisema.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makalla ambaye alioneshwa kuguswa na jambo hilo aliomba mwanasheria wa serikali kutoa ufafanuzi wa jambo hilo ambapo mwanasheria wa serikali Basil Namkambe alisema suala hilo limefika ofisini kwake.
‘’Jambo hili limefika ofisini, namfahamu huyu mzee amekuja mara nyingi kufuatilia suala lake, aligongwa na gari la Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya,’’alisema Wakili Namkambe.
Mheshimiwa Makalla aliagiza ufuatiliaji wa karibu juu ya suala la mlemavu huyo ili lipatiwe ufumbuzi.
Mwaka 1980 aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya alikuwa ni marehemu Azan Eljabri.
Aidha Makalla ambaye alitumia muda mrefu kusikiliza kero za wananchi juu ya matatizo ya ardhi, afya, elimu na miundo mbinu aliwataka watendaji na wanasiasa kushirikiana na wananchi kutatua kero zinazowakabili.
‘’Yote yaliyoelezwa hapa yana uwezo wa kupatiwa ufumbuzi, tutumie kikao hiki kuona matatizo yaliyopo yanatafutiwa ufumbuzi, tarehe 4 Julai, nitaapisha Ma-DC nitawapa maelezo kuhusu ufuatiliaji na usikilizaji kero za wananchi kila Alhamisi,’’alisema makalla
Picha na habari(Rashid Mkwinda)
0 maoni:
Chapisha Maoni