Zaidi ya
ekari 250 za mazao mbali mbali yakiwemo mahindi,mtama,karanga na
alizeti katika kata ya Ibaga,tarafa ya Kirumi,wilayani Mkalama
yameharibiwa na wanyama waharibifu waitwao ngedere na hivyo kusababisha
wakulima wengi kutofikia malengo waliyojiwekea ya mavuno yao
waliyotarajia.
Ngedere
hao wanaokadiriwa kufikia zaidi ya 20,000 wamekuwepo katika kata ya
Ibaga,tarafa ya Kirumi,Wilayani Mkalama na kuendelea kuwasumbua wakulima
wa mazao hayo kwa kipindi cha takribani kati ya miaka saba hadi minane
sasa.
Akitoa
ufafanuzi wa swali lililoulizwa kwa Mbunge wa jimbo la Iramba
Mashariki,Allan Kiulla na mkulima wa Kijiji cha Ibaga,Mwendomgelwa Kingu
aliyetaka kufafamu serikali imejipangaje kuondoa kero ya wanyama hao
waharibifu,diwani wa kata ya Ibaga,Salumu Abdallah Lindi alibainisha
kuwa kero hiyo inatokana na Halmashauri ya wilaya ya Mkalama kutokuwa na
wataalamu wa idara ya wanyamapori wa kupambana na wanyama hao
waharibifu.
Aidha
Lindi akizungumza katika mkutano ulioitishwa na mbunge huyo kwa lengo
la kuwashururu wananchi kwa kumchagua ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero
zao zinazowakera uliofanyika katika Kijiji cha Ibaga,alisema wanyama
hao wanaokadiriwa kufikia 20,000,wana zaidi ya miaka saba hadi minane
kwenye eneo hilo na wanaendeleo kula mazao ya wananchi.
Kwa
mujibu wa mwakilishi huyo wa wananchi tangu alipoingia madarakani mwaka
2015,alishatoa taarifa kwa afisa mazingira wa Halmashauri ya wilaya ya
Mkalama bila mafanikio.
“Tangu
nimeingia madarakani nikiwa kama diwani nilishawasiliana na afisa
mazingira wa wilaya lakini mpaka sasa hivi hakuna juhudi zozote zile
zilizochukuliwa dhidi ya kukabiliana na ngedere hawa”alisisitiza diwani
huyo.
Hata
hivyo Lindi alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya wilaya hiyo
ikiangalie kilio cha wananchi wa kata ya Ibaga na kuhakikisha inamtuma
haraka afisa mazingira ili aweze kwenda kwenye maeneo hayo na kuangalia
uwezekano wa kukabiliana na ngedere hao ambao kwa kiasi kikubwa
wanawaathiri wakulima wao.
Alisisitiza
kwamba wakulima wa maeneo hayo wamekuwa wakiutumia muda wao mwingi
kufukuzana na ngedere hao na kuacha kabisa kushiriki katika shughuli
mbali mbali za mendeleo ya vijiji vyao.
Katika
swali lake la msingi kwa Mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,mkulima wa
Kijiji cha Ibaga,Mwendomgelwa Kingu alimuomba mbunge huyo kuhakikisha
wataalamu wa idara ya wanyamapori wanafika katika kata hiyo kwenda
kuondoa kero ya wanyama hao waharibifu wa mazao.
“Hapa
tumeingiliwa na wanyama wametoroka porini,naomba wahusika waje kwa njia
yeyote ile wawarudishe porini kwa kutumia utaalamu wao wanyama hawa
wanaitwa ngedere”alifafanua mwananchi huyo na mkulima wa Kijiji cha
Ibaga.
Huku
akimshirikisha Mungu katika kula kiapo,Kingu aliweka wazi kuwa pamoja
na kutumia nguvu zao kulima mazao hayo,lakini akaonesha masikitiko yake
kutokana na kugawana mapato ya mazao hayo na wanyama hao.
“Ukweli
tunagawana mapato yetu hasa karanga na mahindi naomba kama mbunge wetu
hili utatusaidiaje,yaani humo wameenea mwote humu tunagawana sana mavuno
yetu,ukiwa kama mbunge hawa wanyama wametoroka”alifafanua mkulima huyo.
Akijibu
hoja za wananchi wa Kijiji cha Ibaga kyhusu wanyama hao
waharibifu,Mbunge wa jimbo la Iramba mashariki,Allan Kiulla aliwataka
wananchi kujenga utamaduni wa kuwatumia viongozi wao kwa kuwapelekea
matatizo yanayowakabili ili waweze kuyashughulikia.
“Sasa
tutumie serikali zetu hawa si ndiyo tuliowachagua sisi wenyewe,hebu
tuwaamini tuwatume kazi…..sawa basi tutafuatilia kwa karibu
wilayani,tutafikisha na mimi leo napita wilayani ntafikisha ujumbe wenu
huu,sawa jamani?alihoji Mbunge Kiulla.
Kwa
upande wake diwani wa viti maalumu,Tarafa ya Kirumi,Habiba Issah
Kununta alimthibitishia mbunge Kiulla kwamba suala la ngedere
linawasumbua kwa kiasi kikubwa wananchi wa kata hiyo.
Hata
hivyo mwakilishi huyo wa wananchi aliweka bayana kuwa wanyama hao
waharibifu wamekuwa wakila mahindi,kwani mara tu wakulima wanapopanda
mbegu,wanyama hao hufukua na kuanza kuzila mbegu hizo.
Alibainisha
Habiba akiwa kama diwani wa viti maalumu Tarafa ya Kirumi alishawahi
kwenda wilayani Iramba kabla ya kugawanywa kuwa wilaya mbili na kutoa
taarifa mara mbili na walipogawanyika alitoa taarifa mara moja,lakini
jibu alilopewa ni kwamba Halmashauri haina afisa mali asili wa
wilaya,kitendo kinachoendelea kuwaumiza sana wananchi.
Akizungumzia
uharibifu wa mazao hayo kwa niaba ya serikali,Afisa Tarafa wa
Kirumi,Juma Salumu Sima alielezea jitihada zilizochukuliwa na serikali
kuwa ni wananchi wenyewe kulinda mashamba yao ili wanyama hao
wasiendelee kuvamia mashamba hayo pamoja na kutoa taarifa kwenye idara
ya wanyamapori ili waweze kufika haraka kuwaondoa wanyama hao.
“Kuhusu
na suala la uharibifu wa wanyama hawa ngedere katika eneo hili la
Ibaga,kweli uchunguzi umefanyika zaidi ya ekari 250 zimeharibiwa na
wanyama wale sababu wao wanakula kwa kuchimba karanga ambazo tayari
zimeshakomaa na kula alzeti iliyokomaa na mahindi mashambani”alifafanua
afisa tarafa huyo.
Aidha
Sima aliweka bayana kwamba kufuatia tathimini iliyofanyika,ni zaidi ya
ekari 250 zimeharibiwa na wanyama hao aina ya ngedere.
Kwa
mujibu wa Sima juhudi walizochukua ni pamoja na wananchi wenyewe
kulinda mashamba yao na kwamba wakulima hao wamekuwa wakiutumia muda wao
mwingi kwa kazi ya kukabiliana na wanyama hao na kuacha kushiriki
katika shughuli mbali mbali za mendeleo.
Hata
hivyo kwa mujibu wa afisa tarafa huyo ni kwamba tayari wamekwishatoa
taarifa wilayani kwenye idara inayoshughulikia wanyamapori ili waweze
kwenda kuwasaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao kutoendelea
kuharibika kutokana na mashambulizi hayo ya ngedere.
0 maoni:
Chapisha Maoni