Jumapili, 17 Julai 2016

MKOA WA PWANI WADHAMIRIA KUWA UKANDA WA UWEKEZAJI NA VIWANDA

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ,amesema amedhamiria mkoa huo kuwa ukanda wa viwanda na uwekezaji  ambapo hadi sasa umetenga maeneo yenye hekta 19,600 na hekari 3,266 kwa ajili ya uwekezaji.
Aidha mkoa huo tayari una viwanda 88 ambavyo ni vikubwa ,vya kati na vidogo huku miradi 10 ya kimkakati ipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,mwishoni mwa wiki iliyopita ,kuhusu hali ya uwekezaji kimkoa,mhandisi Ndikilo ,alisema atavalia njuga suala la uwekezaji ili kuhakikisha mkoa unapiga hatua kiuchumi baada ya miaka mitano.
Alieleza kuwa kati ya viwanda 88 vilivyopo mkoani hapo ni pamoja na wilaya ya Mkuranga na viwanda 41,Chalinze 24,Kibaha mji 10,Bagamoyo viwanda  9,wilaya ya Kisarawe viwili na Mafia 2 viwili.
Mhandisi Ndikilo ,aliainisha maeneo yaliyotengwa katika halmashauri mbalimbali za mkoa ambapo alisema Mji wa Kibaha umetenga hekta 1,450 katika maeneo ya Zegereni,Misugusugu na Mtakuja .
Alisema eneo hilo litakuwa kwa ajili ya viwanda vikubwa na vidogo hekta 318 ambazo zimepimwa na hekta 1,132 zinaandaliwa michoro ya mipango miji.
Alieleza katika halmashauri ya wilaya ya Kibaha imeshatenga hekari 3,266 katika maeneo ya Disunyara yenye hekari 466 na kikongo 2,800.
Mhandisi Ndikilo anasema wilaya ya Kisarawe kuna hekta 4,500 eneo la Visegese ambazo viwanja 291 vyenye ukubwa wa hekari 6 vimepimwa na upimaji unaendelea huku eneo la Vihugwe lenye hekari 2,800 linamilikiwa na Kilua group co.ltd ambalo kwa sasa lipo kwenye harakati za kupata hati miliki .
Alisema Bagamoyo ina hekta 12,500 ambapo eneo la EPZA limetengwa hekta 9,800 ,Mataya hekta 1,200 na Matimbwa hekta 1,500 kwa ajili ya viwanja na kusema tathmini na ulipaji wa fidia unaendelea na tayari eneo la EPZA wananachi 2,180 walifanyiwa thamini na 1,155 wamelipwa fidia zao.
Wilaya ya Mafia alitaja kuna hekta 50 za ardhi katika eneo la Dagoni na huko wilaya ya Mkuranga hekari zilizotengwa ni 7,450 kwa ajili ya viwanda ambako kijiji cha Dundani kuna hekari 700,Misufini,Mponga ,Kidete na Ngalambe 4,000 na Mkiu hekari 1,000.
Rufiji imetenga hekta 1,100 za ardhi katika maeneo ya Utunge huko Utete na imewekwa kwenye ramani ya mji mdogo wa utete kwa ajili ya viwanda.
Mhandisi Ndikilo alisema halmashauri ya Chalinze na Kibiti bado ni changa lakini zimeelekezwa kutenga maeneo ya viwanda ili mkoa ufikie adhama iliyokusudia .
Hata hivyo alieleza kuwa halmashauri nyingine zitaendelea kutenga maeneo ya uwekezaji na kuomba wamiliki wa maeneo makubwa wayaendeleze pasipo kuyaacha pori na endapo yupo atakaekiuka taratibu za kufutiwa hati zao zitafanyika.
Wakati huo huo akizungumzia juu ya miradi kumi iliyopo kimkakati aliitaja kuwa ni sanjali na kiwanda cha vigae kiitwacho Goodwill Tanzania ceramic co.ltd na Mohammed kilua group ambacho kitakuwa suluhisho katika upatikanaji wa nondo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kiwanda kingine ni  cha kusindika matunda na kuyaongezea thamani cha Sayona fruits kinachotarajiwa kujengwa kijiji cha Mboga -Chalinze mwekezaji ni makampuni ya MMI group ambayo yatawekeza fedha za kimarekani mil.55.
Kiwanda kingine ni cha saruji mamba cement kitakachojengwa kijiji cha Magulumatali na Talawanda wilayani Bagamoyo mwekezaji ni MMI group nao kibali wameshapata wakati wowote ujenzi utaanza.
Kiwanda cha nondo cha MMI kitakajengwa eneo la Zegereni halmashauri ya mji wa Kibaha na mradi wa bandari ya nchi kavu na maeneo ya viwanda tayari upimaji wa eneo hilo na tathmini ya mazingira na kumtambua mwendeshaji wa mradi utakapokamilika umeshafanywa .
Mradi mwingine ni wa Eco energy uliopo wilayani Bagamoyo ambao upo kwa ajili ya kuzalisha tani 150,000 ya sukari na megawatts 34 za umeme kwa mwaka na sasa wanawasiliana  na serikali ili kujua hatua zinaendelea kuchukuliwa juu ya mradi huo.
Mhandisi Ndikilo ,alisema mbali na mkoa huo kuvutia wawekezaji pia wanasimamia na kuhakikisha wananchi wanalipwa fidia sambamba na kuondoa urasimu kwenye halmashauri katika mahitaji mbalimbali ya wawekezaji.
Alisema wanahakikisha miundombinu ya maji ,umeme na barabara inaboreshwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji mkoani Pwani.

Mwisho

0 maoni:

Chapisha Maoni