MKUU
wa wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Godwin Gondwe (pichani) amewataka
wafanyabiashara kuhakikisha wanawekeza kwenye kilimo kikubwa cha kisasa
ambacho kitakuwa na tija kwao ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo
na kukuza uchumi.
Gondwe
alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa
dini ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka kuona umuhimu wa kutumia
fursa ya uwepo wa rutuba nzuri ya ardhi iliyopo wilayani humo kujikita
kulima kisasa ili kuweza kupata mafanikio.
Alisema
kuwa lazima wafanyabiashara watambue kuwa kilimo ndio njia pekee ambayo
inaweza kuwainua kiuchumi na kuharakisha kasi ya ukuaji wa maendeleo
iwapo watazingati na kukipa kipaumbele kila wakati
“Niwaombeni
suala la kilimo mlipe msukumo mkubwa sana kwani hii ndio njia pekee
ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kusukuma gurudumu la
maendeleo kwa wilaya yetu”, alisema.
Aidha
pia alisisitiza umuhimu wa wananchi wa wilaya hiyo kutilia mkazo kulima
mazao yanayostahimili ukame ikiwemo Alizeti, Ufuta,Viazi na Mihogo ili
kuweza kukabiliana na tatizo la kutoku patikana mvua za uhakika kwa
ajili ya kilimo cha mahindi.
“Ninajua
katika kipindi hiki tumelima kwa wingi lakini hali ya hewa sio nzuri na
mvua nazo zimekuwa hazipatikana kwa uhakika hivyo lazima wakulima
tubadilike kwa kuanza kupanda mazao yanayostahimili ukame ili kuweza
kuepukana na baa la njaa”, alisema DC Gondwe.
Sambamba
na hayo,Mkuu huyo wa wilaya alizishauri taasisi za kibenki wilayani
humo kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wawekezaji wa kilimo ili waweze
kuzalisha kwa wingi mazao ambayo yataweze kuinua kiuchumi lakini pia
kuchangia pato la Taifa.
Hata
hivyo, Mkuu huyo wa wilaya alitumia pia fursa hiyo kuwaasa wakulima
waliopata mazao kidogo kuhakikisha wanayatunza na kuacha kuyauza kwani
kufanya hivyo kutaweza kusababisha hali ya njaa kwao
Naye
Shekhe wa wilaya ya Handeni, Shabani Mohamed alisema kuwa wao
watamuombea dua Mkuu huyo wa wilaya ili mungu amuwezeshe kuweza kutimiza
majukumu yake ipasavyo na kusaidia kuchangia juhudi za maendeleo kwa
wananchi.
“Nikuambie
Mh Mkuu wa wilaya ujio wako hapa Handeni watu wengi wamefurahi sana
kwani uchapakazi wako unafahamika tokea ulipokuwa unafanya kazi kwenye
kituo cha ITV na tunaamini uhodari huo pia utasaidia kuinua uchumi wetu
“alisema
Alisema
kuwa wao watahakisha wanampa ushirikiano wa hali ya juu ili kumuwezesha
kutekeleza vema majukumu yake ya kuipa maendeleo wilaya hiyo.
Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha.
0 maoni:
Chapisha Maoni