|
MUFTI wa
Tanzania, Shehe Abubakar Zuberi, amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu
kumuombea Rais John Magufuli aweze kuongoza nchi kwa misingi ya haki na
kutunza rasilimali ziwanufaishe Watanzania wote. Aidha, amewataka kuacha
kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawajibike kwa tija na kuleta
matokeo chanya.
Mufti
alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati akifungua semina elekezi ya
viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), iliyohusisha
mashehe wa mikoa, wenyeviti wa halmashauri na makatibu wa mikoa
mbalimbali nchini.
Alisema
kuna umuhimu wa viongozi hao kuielimisha jamii umuhimu wa kufanya kazi
na kujishughulisha katika kutafuta riziki halali na kuachana na tabia ya
kutafuta kwa njia ya dhuluma kwa kuwa hata Mungu hapendi.
“Kauli ya
Rais inasema ‘Hapa Kazi Tu’ tunatakiwa kuisimamia kwa kuwajibika na
kuitekeleza. Tujitume katika ajira zetu na biashara ili tupate riziki ya
halali katika njia zinazompendeza Mwenyezi Mungu,” alisema Sheikh
Zuberi.
Katika
hatua nyingine, Mufti aliwataka viongozi hao kujenga umoja, mshikamano
na kusahau hitilafu walizonazo. Pia waangalie namna ya kutatua
changamoto mbalimbali zilizopo. “Nyumba ni moja tunayojenga hivyo haina
haja ya sisi viongozi na waumini wetu kugombea fito, tutambue kuwa sisi
kama viongozi tuna jukumu la kuwajenga waumini ili wawe na tabia njema
za uadilifu maana uadilifu umepotea miongoni mwetu,” alisema.
Aidha,
Mufti alizungumzia suala la dawa za kulevya na alisema elimu zaidi
inatakiwa kwa jamii na hasa vijana kwa kuwa ndio waathirika wakubwa.
Mufti Zuberi pia aliwataka waumini wote wa dini hiyo kuwa wazalendo na
kuipenda nchi, huku akihimiza viongozi kutumia majukwaa vizuri kwa
kuhamasisha upendo na mshikamano ili kuendeleza amani iliyopo.
Semina
hiyo ya kwanza kufanyika, iliambatana na mada mbalimbali zikiwamo utiifu
kwa viongozi, utawala bora, uchumi na maendeleo, kubadilika kutoka
kwenye ufanyaji kazi kwa mazoea pamoja na mambo mengine.
Share this article :
0 maoni:
Chapisha Maoni