Serikali
imefungia kituo cha tiba asilia cha Foreplan kinachomilikiwa na Tabibu
Juma Mwaka Juma kwa kukiuka masharti ya kibali alichopewa kwa
kujitangaza kuwa anatoa tiba za kisasa badala ya matibabu ya asilia.
Akizungumza
na Waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Wa Baraza la
Tiba Asili na Tiba Mbadala Dkt. Edmund Kayombo amesema kuwa kituo hiko
kimefutiwa usajili na hakiruhusu kutoa huduma za tiba asilia na Tiba
mbadala kwa jamii kwa kutokidhi masharti ya usajili na kufanya kazi
kinyume cha usajili wake.
“Kuanzia
hivi sasa tumekifutia usajili kituo cha tiba asili na tiba mbadala cha
Foreplan kwa kukiuka masharti ya usajili na hivyo hakiruhusiwi kutoa
huduma kwa jamii na watanzania kwa ujumla”.alisisitiza Dkt. Kayombo.
Aidha
Dkt. Kayombo ameongeza kuwa vituo vingine vilivyofungiwa kutoa huduma
ni pamoja na Tabibu Abdallah Mandai wa Mandai Herval Clinic na kituo cha
Fadhaget Sanitarium Clinic kinachomilikiwa na tabibu Fadhil Kabujanja.
Dkt.
Kayombo aliendelea kwa kusema kuwa, ukiacha waliofungiwa kutoa huduma
pia vipo vituo vilivyofungiwa kwa miezi sita kila kimoja kama vile
tabibu Simon Rusigwa wa kituo cha Sigwa Herbal Clinic na Tabibu John
Lupimo wa kituo cha Lupimo Sanitarium Clinic.
Mbali
na hayo Dkt. Kayombo amesema kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala
zinagusa zaidi maisha na afya za wananchi moja kwa moja na hivyo sio
vyema zikaachwa ziendeshwe kiholela bila utaratibu wa kitaalamu na
kimaadili.
“Kutokana
na huduma hizo kutolewa kiholela, waratibu wote mnatakiwa kufuatilia na
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waganga wote ambao hawajajisajili
na kutoa taarifa katika Ofisi ya Msajili wa Baraza la tiba asili na tiba
mbadala kwa kila hatua iliyochukuliwa” aliongeza Dkt. Kayombo.
Aidha
Dkt. Kayombo amesisitiza kwamba kila mtoa huduma lazima asajiliwe yeye
mwenyewe, wasaidizi wake pamoja na kituo chake cha kutolea huduma
kupitia ofisi za Mganga Mkuu wa Halmashauri husika.
0 maoni:
Chapisha Maoni