Ijumaa, 1 Julai 2016

NDIKILO AWATAKA MADC PWANI KUANDAA MPANGO KAZI

KJ1Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,aliyekaa katikakati kati ya waliokaa kwenye viti,wa kwanza kulia ni mwenyekiti wa CCM mkoani Pwani Mwinshehe Mlao na wengine waliosimama ni wakuu wa wilaya wapya mkoani humo.(Picha na Mwamvua Mwinyi) 
…………………………………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ,amewataka wakuu wa wilaya mkoani humo kuhakikisha kila mmoja anaandaa mpango kazi wake kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ili kukabiliana na changamoto zilizopo katika maeneo yao .
Aidha amewataka wahakikishe wanaongeza pato la mwananchi wa mkoa kwa mwaka kutoka sh.1,253,378 ya sasa hadi kufikia 1,500,000 kwa kutumia kikamilifu fursa zilizopo za uwekezaji ,kilimo,biashara na uvuvi.
Katika hatua nyingine amewaasa wakuu wa wilaya hao kupambana na uhalifu mbalimbali ikiwemo madawa ya kulevya ,ujambazi wa kutumia silaha,mauaji ya albino na uhalifu mwingine ili kulinda amani,usalama na utulivu katika maeneo yao.
Mhandisi Ndikilo alitoa rai hiyo jana mara baada ya kuwaapisha wakuu wa wilaya saba zilizopo mkoani hapo.
Alielezea kuwa lengo la mkoa ni kutoka ulipo sasa hatimae kuvuka kwenye hatua nyingine kimaendeleo na kiuchumi.
“Mkiwa kama makamanda wakuu ,mfanye kazi kwa bidii na kwa ubunifu  kwa kuzingatia falsafa ya serikali ya  awamu ya tano ya hapa kazi tuu,matarajio ni kuona changamoto zilizokuwepo zinafanyiwa kazi “alisema mhandisi Ndikilo.
Aidha mkuu huyo wa mkoa alikemea tabia iliyozoeleka ya kukaa ofisini badala ya kwenda kwa wananchi kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi.
Mhandisi Ndikilo alisema huu ni wakati wa kufanya kazi hivyo  aliwataka viongozi hao kutembelea maeneo hayo hususan vijijini.
‘Inashangaza kuona mtu anakuletea kero yake mkuu wa mkoa wakati viongozi wa ngazi ya chini kuanzia vijijini,mitaa ,wakuu wa wilaya ,watendaji wapo,hivyo tokeni mkawasikilize wananchi “alisema mhandisi Ndikilo.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumpter Mshama alisema amejipanga kukabiliana na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi na atahakikisha tatizo la uhaba wa madawati katika wilaya hiyo linakuwa historia.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,alhaj Majid Mwanga alieleza kuwa wakati umefika wa kupambana na wahalifu sanjali na wanaotumia wilaya hiyo kupenyeza biashara za magendo.
Alhaj Mwanga alisema kwasasa kiama kimefika kwa wahamiaji haramu wanaotumia njia na bahari katika wilaya ya Bagamoyo kwani wamejipanga kikamilifu kupunguza tatizo hilo.
Wakuu wa wilaya walioapishwa katika hafla hiyo ni pamoja na Asumpter Mshama (Kibaha), Shaibu Nunduma(Mafia), Juma Njuwayo(Rufiji),alhaj Majid Mwanga (Bagamoyo ).
Wengine ni Gulamu Hussein Kifu (Kibiti), Filberto Sanga(Mkuranga) mkuu wa wilaya mteule wa Kisarawe Happyness William  alikua na udhuru hivyo hakuweza kula kiapo.

0 maoni:

Chapisha Maoni