NDIKILO ASEMA WAKATI WA PROPAGANDA UMEISHA TUFANYE KAZI
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani
mhandisi Evarist Ndikilo, ametoa rai kwa wananchi mkoani humo kuungana
kwa pamoja na serikali ya awamu ya tano kufanya kazi ili kuinua uchumi
na maendeleo ya mkoa na Taifa kijumla.
Aidha amesema wakati wa
malumbano ya kisiasa na propaganda umekwisha hivyo jamii iwe nyuma ya
mh Rais Magufuli na serikali yake kujenga maendeleo ya nchi.
Akizungumza mara baada
ya kupokea taarifa ya tume ya uchaguzi kutoka kwa afisa uchaguzi tume ya
Taifa ya uchaguzi, Adam Nyando, mkuu huyo wa mkoa alisema wakati wa
kukaa na kuzungumzia itikadi za kisiasa umekwisha kilichobaki ni
kukubaliana na matokeo yaliyotangazwa na sio vinginevyo.
“Walioshinda wameshinda, aliyekosa kakosa, maji yameshamwagika, lakini kwa watanzania wote tumeshinda kwa kuwa tuna amani “
“Nawasihi wote tuungane
kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya Taifa, tuchape kazi ili yote
yaliyoahidiwa wakati wa uchaguzi yapate nafasi kutekelezwa” alisema
mhandisi Ndikilo.
Hata hivyo mhandisi
Ndikilo alielezea kuwa kijumla mkoani Pwani zoezi la uchaguzi mkuu
lilikwenda vizuri hadi kipindi cha kutangazwa kwa matokeo.
Alisema wapo baadhi ya
watu walisema na kufikiri nchi isingetoka salama na ingetumbukia kwenye
machafuko ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu badala yake hali ipo shwari.
Alisema mungu
alituepushia na kutuondoa huko na sasa tupo shwariiii huku CCM ikiwa
imeshinda ambapo Rais wa nchi ni John Magufuli.
Mhandisi Ndikilo
alieleza baadhi ya nchi huwa wakitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa
wenyewe, uvunjifu wa amani ama vurugu nyakati za uchaguzi hivyo kwa
Tanzania haina budi kumshukuru mungu kwa kutuvusha na kuendelea kuwa na
amani.
Awali akimkabidhi mkuu
wa mkoa huyo taarifa ya tume ya uchaguzi afisa tume ya Taifa ya
uchaguzi, Adam Nyando, alisema kwa sasa tume ya uchaguzi inajielekeza
kufanya majukumu mbalimbali ikiwemo elimu ya mpiga kura na zoezi la
uandikishaji wapiga kura.
Alisema majukumu hayo
yataenda sambamba na maandalizi ya mchakato wa kura ya maoni kwa kuanzia
na kurekebisha sheria ya kura ya maoni.
Akieliza anasema
uchaguzi mkuu umemalizika kwa amani na utulivu hivyo tume inaendelea na
majukumu yake mengine kwa maslahi ya Taifa.
Hata hivyo alielezea kuwa zoezi la uandikishaji wapiga kura utakuwa ni endelevu.
Nyando alisema sheria inasema kati ya uchaguzi mmoja na uchaguzi mwingine lazima kuwe na uandikishaji unaofanyika.
Mratibu wa uchaguzi
mkoani Pwani, Shangwe Twamala, alisema changamoto zilizojitokeza katika
uchaguzi mkuu 2015 zitashughulikiwa mapema kabla ya chaguzi zijazo.
Katika Uchaguzi mkuu
uliopita CCM ilishinda majimbo yote 9 ya mkoani Pwani na Rais na makamu
wa Rais Samia Suluhu walishinda kwa kupata kura nyingi dhidi ya vyama
vingine vya upinzani.
0 maoni:
Chapisha Maoni