Swissport Tanzania Plc, ambayo ni kampuni inayoongoza kwa kutoa huduma bora za kupakia na kupakua mizigo na kuhudumia abiria duniani, imeboresha huduma zake baada ya kujenga bohari ya kwanza ya kisasa katika bara la Afrika iliyogharimu shilingi bilioni 26 za kitanzania.
“Matarajio ya ukuaji wa huduma za usafirishaji kwa ndege yatakuwa ni ndoto kama hakuna huduma bora za kupakia na kupakua mizigo nchini,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Bw Gaudence Temu wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembea ofisi za Swissport zilizopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam.
Sekta ya usafiri wa anga ni nyeti, ambayo uwepo na ukuaji wake unategemea huduma zinazoaminika—kama vile pamoja na mambo mengine utunzaji na usimamizi wa mizigo, bohari, utunzaji na usimamizi wa barua, utunzaji wa nyaraka zinazohusu mizigo iliyopakiwa au kupakuliwa.
Bw Temu alisema kwamba uzinduzi rasmi wa jengo hilo jipya la kuhudumia mizigo inayoingia na kutoka nchini litazinduliwa rasmi mwezi ujao baada ya ujenzi wake wote kukamilika rasmi.
Alisema kwamba kampuni hiyo Swissport ni ya kimataifa ambayo inatoa huduma zake kwa takribani nchini 58 duniani kwa kiwango cha ubora wa kimataifa ya kusafirisha, kuhifadhi na kupokea mizigo ya aina zote na bidhaa mbalimbali.
Bw Temu aliongeza kwamba kitengo cha bohari ya kupakia mizigo kimetengenezwa kwa teknolojia ya juu kabisa katika kuhakikisha ufanisi na uharakishaji wa upakiaji mizigo ambapo kinaweza kupakia tani 30 kwa siku.
Kwa kutambua umuhimu wa huduma Kampuni ya Swissport inayotoa, Bw Temu alisema: “Tumeamua kuboresha huduma zetu za kupakia na kupakua mizigo…kwa kweli, hizi ni nguzo muhimu kwa ukuaji endelevu wa hii sekta nchini Tanzania.”
Akielezea uboreshaji ambao umefanyika, Bw Temu alisema kwa sasa chumba maalum cha baridi cha Swissport kimepanuliwa kwa kuongeza huduma mpya kama vile mfumo wa ukaguzi wa mizigo ndani ya chumba chenye mitambo maalum. Alisema “chumba hiki maalum kimegawanywa katika maeneo mawili: eneo moja lina ukubwa wa mita 200 za mraba na lingine ni mita 100 za mraba.”
 Akifafanua zaidi, ofisa mkuu huyo wa Swissport alisema kampuni yao imefunga mizani ya futi 20 katika eneo lao kwa kutoa huduma kulingana na mahitaji ya shirika la ndege husika.
Kwa upande wa kuhifadhi mizigo, kampuni ya Swissport imejenga bohari ya kisasa na salama na inayoweza kufiwa kwa urahisi. Imefungwa mitambo maalum ya CCTV na ya ukaguzi wa magari. Pamoja na mambo mengine, bohari hii ina vifaa maalum kwa ajili ya ukaguzi, uangalizi na utunzaji salama wa mizigo.
Uboreshaji uliofanywa hivi karibuni umefanywa kwa lengo la kuisaidia serikali katika jitihada zake za kuboresha huduma za usafiri wa ndege, ambao ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi na kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi za ustawi wa mamilioni ya Watanzania, kwa mujibu wa Meneja Mikataba na Masoko-Swissport, Bw James Mhagama.
swissprt-2Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Swissport, Bw Gaudence Temu akiwaelezea waandishi wa habari waliofanya ziara katika jingo hilo jipya la bohari ya kipekee Afrika jinsi inavyofanya kazi ya kuhifadhi, kupakia na kupakua mizigo na bidhaa mbalimbali iliyojengwa na kampuni katika jitihada za kuboresha huduma zao katika kiwanja cha ndege cha Mwl nyerere
swissportAfisa Mtendaji Mkuu wa Swissport Tanzania, Bw Gaudence Temu jinsi sehemu ya kutolea mizigo ya ndani inavyofanya kazi kwa ufanisi katika jengo hilo jipya la kisasa.