…………………………………………..
Serikali
itaendelea kusimamia haki ya mtoto wa kike ya kupata elimu na
kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwapeleka mahakamani wale
wote wanaowapa ujauzito wanafunzi na kuwakosesha kupata elimu ambayo ni
haki yao ya msingi.
Kauli
hiyo imetolewa na Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Seriklali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo alipokuwa akijibu swali la
nyongeza la Janeth Mbene wa Ileje baada ya kujibu swali la msingi
lililohoji kuhusu kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.
“Serikali
haitamvumilia mwanaume yeyote atakayempa ujauzito mwananfunzi na
kukwamisha kupata elimu kwa wakati na kumharibia malengo ya maisha yake”
alisema Naibu Waziri Jafo.
Hatua
hiyo ya Serikali itawahakikishia na kuwawezesha watoto wa kike nchini
kusoma na kumaliza masomo yao hatua ambayo itakuwa msaada kwa watoto hao
wa kike, familia zao na taifa kwa ujumla.
Akisistiza
msimamo wa Serikali kuhusu wanaume wanaowapa ujauzito wanafunzi, Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
alisema kuwa Serikali haipo tayari kuwavumilia wanaume wenye tabia ya
kuwakwamisha watoto wa kike kupata elimu kwa kuwapa ujauzito na
itahakikisha sheria inachukua mkondo wake ili kukomesha tabia hiyo.
Akizungumzia
tatizo hilo la wanafunzi kupata ujauzito wakiwa shuleni, Mbunge wa
Jimbo la Igunga Seif Khamis Gulamali alisema kuwa tatizo hilo lipo
sehemu mbalimbali nchini ambapo watoto hubebeshwa mimba wakiwa katika
umri mdogo wa kuwa shuleni na tatizo hilo linaendelea kuleta hasara
kubwa kwa wanafunzi wenyewe, familia zao na taifa kwa ujumla.
Gulamali
alisema kuwa hali hiyo inatokana na hulka ya makabila mengi nchini hasa
ya wafugaji hali inayosababishwa na tabia ya kuhama hama kutafuta
malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao.
“Wapo
wazazi wanaowapa maelekezo watoto wao wasifaulu mitihani yao ili waweze
kuolewa na wamegeuzwa kuwa sehemu ya kipato cha familia zao kwa kupata
mahari” alisema Gulamali.
Ili
kukomesha tabia hiyo ya kuwapa ujauzito watoto wenye umri mdogo hasa kwa
wafugaji, Gulamali alisema kuwa ipo haja ya Serikali kupitia Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuweka
mazingira mazuri ambayo yatawapa wananchi wengi fursa ya kuwekeza
kwenye sekta ya kilimo na mifugo kwa kuwahakikishia upatikanaji wa maji
kwa wingi ili wananchi wazalishe na kuondokana na tabia ya kuhama hama
kwa wazazi wao ambayo imekuwa kikwazo kikubwa kwa watoto kupata elimu.
Kuhusu
shilingi milioni 50 zilizoahidiwa na Serikali kwa kila kijiji hapa
nchini, Gulamali alisema kuwa ni vema ufikiriwe mfumo wa kupeleka hizo
fedha ambao utakuwa wa tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla
utakaohkikisha fedha hizo zitakuwa endelevu na kuwarahisishia wananchi
kazi na kuongeza uzalishaji wa mazao yatakayowaongezea kipato.
Hatua
hiyo itasaidia taifa kuwa na matumizi bora ya rasilimali fedha
zinazotolewa na Serikali kwa kuwekeza kwenye sekta za viwanda, mifugo,
uvuvi na kilimo ambapo Tanzania kuna mvua ya kutosha, mabonde yenye
rutuba, mito, maziwa, bahari pamoja na watu ambao ndio msingi wa
maendeleo kwa taifa kwa kuongozwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ifikapo
2025 Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati.
0 maoni:
Chapisha Maoni